Vitongoji vitatu Tandahimba vyakosa wagombea, uchaguzi waahirishwa

Muktasari:

  • Vitongoji vitatu katika kijiji cha Ruheya halmashauri ya wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara nchini Tanzania vimeshindwa kufanya uchaguzi baada kutojitokeza kwa wagombea wa chama chochote kuwania nafasi hizo pamoja na nafasi ya mwenyekiti wa kijiji hicho

Tandahimba. Vitongoji vya Paris, Rahaleo na Ruheya katika kijiji cha Ruheya wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara nchini Tanzania vimeshindwa kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika leo Jumapili Novemba 24, 2019 baada ya kutojitokeza wagombea wa chama chochote kwa ajili ya kuchukua fomu kuwania nafasi hizo.

Akizungumza na Mwananchi, Msimamizi wa uchaguzi halmashauri ya wilaya ya Tandahimba, Ahmad Suleiman amesema jumla ya nafasi za vitongoji zilizokuwa zinagombewa ni 650 ambapo nafasi 646 CCM imepita bila kupingwa baada ya vyama vilivyokuwa vinashiriki uchaguzi kujiondoa na nafasi moja inagombewa leo (kitongoji cha Kiwanjani)

Pia, amesema uchaguzi umeahirishwa katika kijiji hicho cha Ruheya ambako wagombea hawakujitokeza kuwania nafasi hiyo.

“Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka 2019 tarehe tano lilitolewa tangazo la kuahirishwa kwa uchaguzi eneo hilo mpaka Desemba 15 ambapo tutaanza tena suala la uchaguzi kwa kijiji cha Ruheya na vitongoji vyake,” amesema Suleiman

Katika halmashauri ya Tandahimba ilikuwa na jumla ya nafasi za vitongoji 650 vilivyokuwa vinagombewa ambapo CCM imepita bila kupingwa katika vijiji 646, na vijiji vilivyokuwa vikigombewa ni 143 ambapo vijiji  142 CCM imepita bila kupingwa na kijiji kimoja uchaguzi umeahirishwa