VIDEO: Vituo 25 vitakavyotumika kuchukua sampuli za corona Dar hivi hapa

Muktasari:

Mkoa wa Dar es Salaam umetoa orodha ya vituo 25 vya afya vilivyotengwa kwa ajili ya kuchukua sampuli ya vipimo vya ugonjwa wa homa  ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19).

Dar es Salaam.  Mkoa wa Dar es Salaam umetoa orodha ya vituo 25 vya afya vilivyotengwa kwa ajili ya kuchukua sampuli ya vipimo vya ugonjwa wa homa  ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19).

Kwa mujibu wa taarifa ya mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda iliyotolewa leo Jumatano Aprili 15, 2020 imeeleza kuwa vituo hivyo vitatumika kuchukua sampuli za wanaoshukiwa.

Taarifa hiyo imesema kuwa baada ya sampuli kuchukuliwa kwenye vituo hivyo zitapelekwa kwenye maabara kuu ya Taifa

“Mkoa umejipanga kupunguza ueneaji wa ugonjwa kwa kuainisha vituo maalum vya wahisiwa wanaokidhi vigezo vya tafsiri ya ugonjwa, kuchukuliwa sampuli kwa ajili ya vipimo vya maabara katika maabara kuu ya Taifa” imesema taarifa hiyo ya Makonda kwa umma.

“Vituo hivi havitatumika kupima sampuli, bali ni vituo vya kukusanyia sampuli za wahisiwa tu. Aidha, vituo hivi vipya vitawawezesha wahisiwa kupata huduma ya vipimo kwa kuchukuliwa sampuli katika maeneo yao ya karibu kabla ya kuchangamana na watu wengine na kusababisha kusambaza virusi hivyo.”

Taarifa hiyo imesema kuwa manispaa ya Kinondoni itatumia vituo sita vikiwemo hospitali za Mwananyamala, Magomeni, Mikoroshini, IST, TMJ na Rabininsia.

Manispaa ya Ilala vituo vitakavyotumika ni Amana, Buguruni, Mnazi mmoja, Muhimbili, Hindu Mandal, Aga Khan na Regency.

Vituo vingine vilivyoteuliwa katika manispaa ya Temeke ni hospitali ya Temeke, Mbagala Rangi Tatu, Yombo na TOHS.

Vituo vitakavyotoa huduma hiyo katika manispaa ya Ubungo ni pamoja na Sinza, Kimara, Mloganzila na Bochi na manispaa ya Kigamboni vitatumika vituo vitatu vya  Vijibweni, Kigamboni na Agha Khan.

Hata hivyo katika orodha hiyo kituo kimoja manispaa ya Ilalal hakikutajwa jina.