Vituo vya kuchakata majitaka kujengwa Dar

Muktasari:

Kituo cha kukusanya majitaka chenye thamani ya Sh800 bilioni kujengwa jijini Dar es Salaam. Kituo hicho kitabadili maji hayo na kuyarudisha kumwagilia miti na bustani
 

Dar es Salaam. Katika kukabiliana na changamoto ya maji taka, Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania upo kwenye mpango wa kuanzisha vituo maalum kwa ajili ya kuchakata maji taka na kuyarudisha kwenye matumizi.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kituo cha kuanzia kitajengwa eneo la Jangwani na kitagharimu Sh800 bilioni.

Makonda ameyasema hayo leo Jumatatu Novemba 18, 2019 alipokutana na viongozi wa dini kwa lengo la kuwaeleza utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyotekelezwa katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa awamu ya tano wa Serikali ya Tanzania.

Makonda amesema kituo hicho kitakusanya maji taka kutoka maeneo ya Kariakoo, Upanga, Posta na mitaa mingine ya katikati ya Jiji hilo.

“Baada ya maji hayo kukusanywa, yatabadilishwa na kubadilishwa matumizi. TutatumiA kumwagilia miti na bustani za jiji hili. Katika nchi nyingine wanaweza hata kutumia kwenye kupikia.”

“Mimi ndio nilimshauri rais tuanze kwa kumwagilia miti maana watu wasingetuelewa kwamba maji haya yatumike kupikia,” amesema Makonda

Makonda amesema kituo hicho ni miongoni mwa vituo vikubwa vitatu vitakavyojengwa Dar es Salaam katika kuhakikisha maji taka yanakusanywa.

Kando na vituo hivyo vikubwa, Makonda amesema vitakuwepo pia vituo vidogo 50 lengo ni kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2020 ukusanyaji wa majitaka ufikie angalau asilimia 40.

Katika mkutano huo, Makonda amewaomba viongozi hao wa dini kuwakumbusha waumini wao kuwaheshimu watu walioapa kulinda nchi na usalama wao.

Amesema polisi na wanajeshi wanafanya kazi kubwa kuhakikisha mkoa unakuwa na amani huku ulinzi na usalama vikitawala.

 

 

Makonda amesema polisi wamefanya kazi kubwa kuondoa vitendo vya uhalifu katika jiji hilo ambalo lilikuwa lina matukio mengi.

“Kulikuwa na ujambazi zamani watu walikuwa wanauwawa hovyo, wakati mwingine hata polisi walikuwa wanashambuliwa lakini sasa kazi kubwa imefanyika kuna utulivu, hakuna panya road wala wizi wa vifaa vya magari,” amesema

“Mikakati mingi iliwekwa na (Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam-Lazaro) Mambosasa na wenzake na matokeo tunayaona jiji la Dar sasa ni shwari,” amesema

Mkuu huyo wa mkoa amesema kabla hajalala kila siku amejipa jukumu la kuuombea mkoa huo na anapoamka asubuhi anashukuru kwa ajili ya wananchi wake kuwa salama.