Vituo vya mafuta Tanzania vyatakiwa kubandika bei ya bidhaa hiyo

Muktasari:

Vituo vyote vya mafuta nchini Tanzania vimetakiwa kuchapisha bei za mafuta katika mabango yanayoonekana ili kuwafanya wateja kununua katika sehemu yenye unafuu wa bei, kwamba bila kufanya hivyo nikosa kisheria.

Dar es Salaam. Vituo vyote vya mafuta nchini Tanzania vimetakiwa kuchapisha bei za mafuta katika mabango yanayoonekana ili kuwafanya wateja kununua katika sehemu yenye unafuu wa bei, kwamba bila kufanya hivyo nikosa kisheria.

Hayo yamebainishwa katika taarifa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) iliyotolewa leo Jumatano Agosti 7, 2019 ambayo pia imetangaza kushuka kwa bei ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa yanayoingizwa nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ikilinganishwa na toleo lililopita la Julai 3, 2019.

 

Licha ya kuwepo kwa punguzo la zaidi ya Sh100 katika baadhi ya maeneo lakini kampuni zimeruhusiwa kuweka bei za ushindani ila zisizovuka bei za ukomo zilizowekwa na Ewura.

“Mbali na kuweka bei za ushindani lakini pia ni lazima wauzaji watoe risiti za mauzo kutoka kwenye mashine za kielektroniki (Electrical fiscal pump printer) na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo zikiwa na jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita,” inaeleza taarifa hiyo.

Inabainisha kuwa stakabadhi hizo zitatumika kama kidhibiti endapo kutatokea malalamiko ya kuuziwa mafuta kwa bei juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora kinachofaa.

“Bei kikomo za mafuta kwa kila eneo zinapatikana pia kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *152*00#  na kisha kufuata maelekezo na inapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkononi,” inaeleza.

Wakati  bei ya mafuta ikishuka katika maeneo mengi nchini, MKkoa wa Kigoma bado unaongoza kwa kuwa na bei kubwa huku Mkoa wa Dar es Salaam ukiwa na bei ndogo kuliko maeneo mengine.

Kigoma bei ya ukomo ya lita moja ya mafuta ya Petroli ni Sh2,384, dizeli Sh2,339 na mafuta ya taa ni Sh2,318 ikilinganishwa na Dar es Salaam ambako bei zake ni Sh2,153, Sh2,107 na Sh2,086 katika mtiririko ule wa awali.

Hiyo inamaanisha kuwa mnunuzi wa lita moja ya mafuta ya petroli katika Mkoa wa kigoma atalipa Sh231 zaidi ya mnunuzi wa Dar es Salaam na atalipa Sh232 zaidi kwa mafuta ya taa na dizeli.