Viwanja vidogo vya ndege 208 vyafungiwa Tanzania

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari

Muktasari:

TCAA  yatangaza kuvifungia viwanja vya ndege vidogo 208 vilivyopo katika mikoa mbalimbali nchini. Yasema vimeshindwa kufuata kanuni  ya 323 na kanuni nyingine za usafiri wa anga za viwanja vya ndege za mwaka 2017.

Dar es Salaam. Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari ametangaza kuvifunga viwanja vidogo vya ndege 208 baada ya kubainika kushindwa kufuata kanuni ya 323 na kanuni nyingine za usafiri wa anga za viwanja vya ndege za mwaka 2017.

Amesema kanuni hizo zinakataza uendeshaji wa viwanja vya ndege bila kupata usajili au leseni inayotolewa na TCAA  na ni kosa linaloadhibiwa kisheria.

Johari ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Desemba 23, 2019 wakati akizungumza na wanahabari, akisema viwanja hivyo 208 vimeondolewa katika rejista ya viwanja vya ndege na havitaruhusiwa kutumika bila idhini ya TCAA.

"Tulifanya uhakiki wa miezi mitatu kwa kutumia ndege maalumu kuviangalia viwanja hivyo ambapo tumebaini ni mapori tu. Tuna viwanja vya ndege  vidogo 643 kati hiyo 208 tumevifungia na tutaweka katazo," amesema Johari.

Johari amesema Mei 6, 2019 ilitoa muda hadi Desemba 31, 2019 kwa wamiliki au waendeshaji wote wa viwanja  ndege vidogo kutimiza matakwa ya kanuni na kusajili au kupata leseni.

"Mamlaka inawapongeza wote walioitikia wito na imepokea maombi ya kuongeza muda hadi Machi 31 mwaka 2020  kwa wale waendeshaji wa viwanja vidogo 120 waliomba  kwa ajili ya mchakato huu," amesema Johari.

Kwa mujibu wa Johari, viwanja hivyo vipo mikoa ya Arusha, Pwani, Dodoma, Mwanza,  Shinyanga,  Mara, Tanga, Singida,  Tabora, Morogoro, Rukwa, na Ruvuma.