Vodacom Tanzania kusajili laini za simu mpaka saa mbili usiku

Muktasari:

Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema Desemba 31, 2019 itakuwa mwisho wa matumizi ya laini za simu kutumika ambazo hazitakuwa zimesajiliwa kwa alama za vidole.

 Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku nane kabla kuzimwa, kampuni ya Vodacom Tanzania imeongeza muda wa kufanya kazi kuhakikisha inawasajili wateja wengi zaidi kwa alama za vidole.

Kampuni hiyo inayohudumia zaidi ya watu milioni 15.3 hivyo kuongoza kwa wateja wengi imesema imeongeza muda huo ili kutoa nafasi kwa wananchi wenye namba au kitambulisho cha Taifa kutimiza wajibu wao katika zaidi ya maduka 400 pamoja na madawati ya huduma nchini kote.

Leo Jumapili Desemba 22, 2019 Mkurugenzi mtendaji wa Vodacom, Hisham Hendi amesema hatua hiyo inakusudia kuwanusuru wateja wanaokidhi vigezo kukosa huduma kuanzia Januari Mosi baada ya siku ya mwisho kupita.

“Tumeongeza saa za kazi kuwapa wateja wetu wenye vitambulisho vya Taifa au namba ya kitambulisho cha Taifa kutii sheria. Wautumie msimu huu wa sikukuu kusajili laini zao kwa alama za vidole,” amesema Hendi.

Amewasisitiza wateja ambao hawajaomba au kukamilisha utaratibu wa kupata kitambulisho cha Taifa wafanye hivyo haraka ili wasikose huduma za mawasiliano siku ya mwisho itakapofika.

Mapema Mei 2019 Serikali ya Tanzania ilianzisha usajili wa laini zote za simu kwa alama za vidole wenye lengo la kuwafahamu wateja hivyo kuzuia utapeli na uhalifu mwingine wowote.

Usajili huo unakamilika wiki ijayo, Desemba 31, 2019 na watakaokuwa hawajafanya hivyo watazimiwa huduma.

Mpaka katikati ya Desemba 2019, takwimu za Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) zilikuwa zinaonyesha zaidi ya wateja milioni 19.6 kati ya milioni 47 waliopo walikuwa wamesajili laini zao kwa mfumo huo.

Vodacom kwa upande wake ilikuwa imesajili wateja milioni 6.2 ambao ni sawa na asilimia 40 ya watu inaowahudumia.

Kuhakikisha hakuna anayeachwa nje ya mawasiliano kwa kutosajili laini yake, Hendi amesema mawakala wao wenye Vodacom vitambulisho na mavazi maalumu watapita kwenye makazi ya wananchi, ofisi na  biashara kusajili laini za simu.

“Sio lazima kuwa na kitambulisho cha Taifa, wenye  namba ya kitambulisho pia tunawasajili,” amefafanua Hendi akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi zaidi.