Vyama 7 vilivyojitoa uchaguzi wa mitaa vyatoa tamko la pamoja

Muktasari:

Vyasema vinaendelea na mashauriano, hivyo Watanzania wawe tayari kusubiri maelekezo

Dar es Salaam. Siku moja kabla ya kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuanza vyama saba vilivyojitoa katika mchakato wa uchaguzi huo vimetoa tamko vikiwataka Watanzania kujiandaa kwa maelekezo mengine yatakayotolewa baada ya kumalizia mashauriano.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Novemba 16 baada vyama vya Chadema, ACT-Wazalendo, Chaumma, CCK, NCCR Mageuzi, UPDP na NLD kutoa msimamo wao.

Akiongea kwa niaba ya vyama hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari amesema vyama hivyo vilishatoa matamko ya kujitoa kwenye uchaguzi huo kutokana na ukiukwaji wa kampuni na sheria.

Amesema baada ya vyama hivyo kujitoa kushiriki uchaguzi, serikali kwa upande wake ilitoa matamko mbalimbali yaliyokuwa yakitofautiana na kuchanganya, licha ya kuwa yalikuwa yakitolewa na mtu mmoja ambaye ni Waziri wa Tamisemi.

"Baada ya wagombea wa vyama hivyo kujitoa kwenye uchaguzi huo, waliwajulisha wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kuhusu kujitoa na kwa ngazi ya Taifa baadhi ya vyama vilimjulisha waziri wa Tamisemi kwa barua,” amesema Profesa Safari.

Baada ya kushauriana vyama hivyo vimeazimia kwa pamoja havitashiriki kwa vyovyote “kwenye kampeni na uchaguzi unaoenda kinyume na kanuni za uchaguzi” na vimewataka wanachama na wafuasi kutoshiriki.

Aidha vyama hivyo vimetoa wito “uchaguzi huo ufutwe na mchakato wake uanze upya kwa mustakabali wa amani ya Taifa.”

"Tunatoa wito kwa umma na Watanzania wajiandae kwa maelekezo yoyote yatakayotolewa baada ya mashauriano yanayoendelea miongoni mwa vyama na makundi mengine ya jamii," amesisitiza Profesa Safari.

Maazimio mengine ni pamoja na kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia uchaguzi zote nchini.

Amesema vyama hivyo vimetambua kauli na wito uliotolewa na viongozi wastaafu na viongozi wa dini nchini na kuwaomba kuchukua hatua za kuingilia kati mapema ili kunusuru amani ya Taifa.

Akizungumza katika mkutano huo, Kiongozi wa ACT –Wazalendo, Zitto Kabwe amesema Watanzania wanatakiwa kuwa tayari na kutega masikio wakati vyama hivyo na makundi mbalimbali yakiendelea na mashauriano.

"Hatutakubali kuendelea kupingwa kwa miaka minne mfululizo. Tunawataka Watanzania kuendelea kutega masikio wakati hatua zikiendelea ikiwemo mashauriano na makundi mbalimbali," amesema Zitto.

Mwenyekiti wa Chaumma, Hashimu Rungwe ametumia mkutano huo kufafanua taarifa zinazoelezwa kuwa vyama vingine vilivyojitoa havikuweka wagombea, akisema si za kweli na akashauri zipuuzwe.

"Mimi niliweka wagombea 25O ambao walitolewa wote wanaosema sikuweka wagombea muwapuze," alisema Rungwe