Vyama vya upinzani vyaeleza vilivyojipanga kampeni uchaguzi Serikali za mitaa

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia Makini Mohamed Abdula

Muktasari:

  • Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini  Tanzania vitakavyoshiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa wameeleza namna watakavyoshiriki kampeni  za uchaguzi huo zilizoanza jana Jumapili Novemba 17, 2019.

Dar es Salaam. Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini  Tanzania vitakavyoshiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa wameeleza namna watakavyoshiriki kampeni  za uchaguzi huo zilizoanza jana Jumapili Novemba 17, 2019.

Vyama vya upinzani vinavyoshiriki uchaguzi huo ni ADC, NRA, Demokrasia Makini, TLP, DP na  AAFP. Chama cha NLD kipo katika sintofahamu baada ya viongozi wake wakuu kuvutana kuhusu kushiriki uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Wakati vyama hivyo vikipanga mikakati, vyama vingine saba vya upinzani havitashiriki uchaguzi huo ambavyo ni  CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi , ACT-Wazalendo, UPDP na Chaumma kwa maelezo kuwa mchakato wa uchaguzi huo umekumbwa na ukiukwaji wa kanuni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, Abdul Mluya ambaye ni Katibu Mkuu wa DP amesema, “tumezindua kampeni zetu jana mkoani Kigoma ambako tuna wagombea saba ngazi ya vijiji.”

“Dar es Salaam hatukuambulia kitu wote walikwenda na maji (kuenguliwa), tutafanya kampeni za jukwaani , nyumba kwa nyumba na mtu kwa mtu ili tuwafikie wananchi wote wa mtaa husika,” amesema  .

Katibu Mkuu wa NRA, Hassan Kisabya amesema chama hicho kitafanya kampeni za jukwaani na nyumba kwa nyumba, akibainisha watajikita zaidi mkoani Kigoma kwa kuwa wana wagombea wengi.

Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia Makini, Mohamed Abdula amesema  chama hicho kitazindua kampeni  zake Novemba 21, 2019  mkoani Morogoro ambako wagombea wao wengi wamepitishwa.

 

Abdula amesema mbali na Morogoro wagombea wao wapo mikoa ya Tabora, Kigoma, Mara na Dar es Salaam.

“Tumeona umuhimu kushiriki uchaguzi huu kwa sababu  kutoshiriki ni sawa na kujiondoa kwenye  mikakati ya kisera na kisiasa. Tuna uhakika wagombea wetu wa Mvomero watashinda ndio maana hatujaona sababu ya kususia,” amesema Abdula.