WHO: Afrika si sehemu ya majaribio chanjo ya corona-VIDEO

WHO: Afrika si sehemu ya majaribio chanjo ya corona-VIDEO

Muktasari:

Mkurugenzi wa Shirika la Afya duniani (WHO),  Tedros Adhanom amesema nchi za barani Afrika hazitatumika kama uwanja wa majaribio ya chanjo ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Shirika la Afya duniani (WHO),  Tedros Adhanom amesema nchi za barani Afrika hazitatumika kama uwanja wa majaribio ya chanjo ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.

Adhanom ametoa ufafanuzi huo kwa vyombo vya habari akisema hivi karibuni alisikia baadhi ya maoni ya baadhi ya wanasayansi kwamba Afrika itatumika kama uwanja wa majaribio ya chanjo ya ugonjwa huo.

Mkurugenzi huyo amelaani kauli hizo na kuziita za kibaguzi, kwamba hazipaswi kupewa nafasi wakati wa vita dhidi ya virusi hivyo.

“Kiukweli nilisikitishwa na kauli hizo, na nikasema tunapohitaji mshikamano hizi kauli za kibaguzi haziwezi kusaidia kwa sababu zipo kinyume na mshikamano. Afrika haiwezi na haitakuwa uwanja wa majaribio ya chanjo yoyote,” amesema Adhanom.

Amebainisha kuwa WHO itafuata kanuni na taratibu zote za kujaribu chanjo au tiba duniani kote kwa kutumia kanuni zake ilizojiwekea wakati wote, bila kujali ni Afrika, Ulaya au popote.

Amesema utaratibu wa chanjo au tiba utakaotumika hata kwa ugonjwa wa corona utakuwa ni uleule unaotumika wakati wote kwa sababu binadamu wote ni sawa na hawapaswi kubaguliwa.

Adhanom amesema WHO haitasahau ubaguzi huo kutokea, kanuni zote za chanjo zitazingatiwa bila ubaguzi kwakuwa binadamu wote ni sawa na wana haki sawa.

Amesema shirika hilo linalaani  kauli hizo zilizotolewa na wanasayansi hao kutaka Afrika itumiwe kama uwanja wa majaribio ya chanjo ya corona,  watahakikishia jambo hilo halitatokea iwe ni Afrika au popote au kwa nchi yoyote.