Waandamanaji 30 wauawa Iraq

Baghdad. Watu 30 wameuawa wakati wa maandamano ya umma yaliyofanyika dhidi ya serikali nchini Iraq.

Mjumbe wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, Faisal Abdullah, amesema vifo hivyo vilitokea wakati polisi iliporusha risasi za moto na gesi ya machozi kuwatawanya waandamanaji.

Watu wanane waliuawa katika mji mkuu Baghdad, wengine 18 katika miji ya Maysan na Dhi Qar, watatu mjini Basra na mmoja katika jimbo la kusini la Muthanna.

Kulingana na Abdullah watu wengine zaidi ya 2,300 walijeruhiwa huku majengo takriban 50 ya serikali na ofisi za vyama vya siasa yakichomwa moto.

Marufuku ya kutotoka nje imetangazwa kwenye majimbo ya Dhi Qar, Basra, Muthanna na Wasit.

 

Ahadi ya mageuzi 

 

Waandamanaji walianza kukusanyika Ijumaa katika eneo la Tahrir mjini Baghdad baada ya hotuba ya waziri mkuu Adel Abdel-Mahdi aliyoitoa kwa njia ya televisheni, akitoa ahadi ya kufanya mageuzi na mipango ya kulifanyia mabadiliko Baraza lake la Mawaziri wiki ijayo.

 

"Kutaka serikali iangushwe bila kuwa na njia mbadala ya kikatiba kutaitumbukiza nchi kwenye machafuko," alisema Abdel-Mahdi.