Wabunge CCM, Chadema wavutana dhana ya ugatuaji wa madaraka

Jaffar Michael Mbunge wa Moshi Mjini Chadema

Muktasari:

Utekelezaji wa dhana ya ugatuaji wa madaraka umeleta mvutano bungeni nchini Tanzania kati ya Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota na Jaffar Michael (Chadema)

Dodoma. Wabunge wa CCM na Chadema nchini Tanzania wamevutana kuhusu utekelezaji wa dhana ya ugatuaji wa madaraka wakati wakichangia katika mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka 2020/2021.
Wabunge hao Abdalah Chikota (Nanyamba-CCM) na  Jaffar Michael wa  Chadema Moshi Mjini walichangia mjadala huo leo Alhamisi  Aprili 9, 2020.
Akichangia Chikota amesema dhana ya ugatuaji ni pana sana na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli inatekeleza kwa dhati.
“Serikali ya awamu ya tano ina nia ya dhati, lengo kubwa ni kupeleka huduma karibu na wananchi hivi vituo 350 vilivyojengwa kazi yake ni kutoa huduma kwa wananchi,”amesema.
Amewataka wabunge kutokariri utekelezwaji kwa kutumia sera ya mwaka 1998 ambao hauwezi kutekeleza kwa namna hiyo kwa sasa.
Hata hivyo, Michael amesema anakubaliana kuwa dhana ya ugatuaji ni pana lakini anachotaka utekelezaji uwe kwa namnna ilivyokuwa Serikali ya Awamu ya Tatu (Ya Rais Benjamin Mkapa).
Amesema utekelezaji anaozungumza ni halmashauri ziweze kujitegemea kwa vyanzo vyake.
“Kila mtu zahanati, anaangalia kituo cha afya hapa bungeni. Lakini kama ingetekelezwa kwa namna hii mngepunguzia Serikali Kuu mzigo. Serikali ya Awamu ya Tatu tulitekeleza, hii ina faida kubwa sana,”amesema.