Wabunge CCM wamkalia kooni waziri Masauni ujenzi vituo vya polisi

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania,  Hamad Masauni

Muktasari:

Wabunge sita wa CCM leo Jumanne Novemba 11, 2019 wamembana naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania,  Hamad Masauni kuhusu ujenzi wa vituo vya polisi katika majimbo yao.

 

Dodoma. Wabunge sita wa CCM leo Jumanne Novemba 11, 2019 wamembana naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania,  Hamad Masauni kuhusu ujenzi wa vituo vya polisi katika majimbo yao.

Wabunge hao Mary Chatanda (Korogwe), Anne Kilango (kuteuliwa), Allan Kiula (Mkalama), Venance Mwamoto (Kilolo), Miraji Mtaturu (Singida Mashariki) na Zuberi Kuchauka (Liwale).

Aliyeanza kuhoji suala hilo katika kipindi cha maswali ni majibu ni Mary aliyetaka kujua kama Serikali itawapa kipaumbele kwa kuwajengea jengo la kituo cha Polisi Wilaya ya Korogwe kwa sababu kiwanja kipo.

Akijibu swali hilo,  Masauni amesema kuna upungufu wa vituo vya polisi katika baadhi ya Wilaya nchini, kuahidi  katika mipango ya ujenzi maeneo mbalimbali, kituo hicho kitajumuishwa.

Katika swali la nyongeza, Mwamoto amehoji ni lini Serikali itapeleka gari kwa ajili ya kituo cha polisi Mbuyuni ili inapotokea ajali waweze kutoa huduma

Akijibu swali hilo la nyongeza,  Masauni amesema gari likipatikana wataangalia uwezekano wa kulipeleka katika kituo hicho.

“Kwa sasa hatuna gari. Namuomba mheshimiwa mbunge avute subira,” amesema Masauni.

Kilango naye alizungumzia jinsi alivyonunua gari kwa ajili ya polisi jimboni kwake lakini hadi leo Serikali imeshindwa kutoa fedha za kulifanyia ukarabati.

“Hadi leo Serikali inashindwa kupeleka fedha kidogo kwa ajili ya kulifanyia ukarabati,” amesema Kilango na kujibiwa na Masauni kuwa watatoa fedha za ukarabati.

Mtaturu amehoji ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa jengo la mkuu wa Polisi jimboni kwake kwa kuwa umechukua muda mrefu.

Katika majibu yake,  Masauni amesema atakwenda katika jimbo hilo kushauriana naye kuhusu ujenzi wa jengo hilo.

Kiula  amehoji lini ujenzi wa jengo la kituo cha polisi Mkalama utakamilika kwa sababu limeanza kuharibika na kujibiwa na Masauni kuwa Serikali inatafuta fedha kumalizia ujenzi huo.