Wabunge majimbo ya Kusini mwa Tanzania wamuangukia Rais Magufuli

Muktasari:

  • Wabunge Nachingwea, Lindi Mjini na Liwale wamemuomba Rais Magufuli kushughulikia changamoto zilizo kwenye majimbo yao.

Dar es Salaam. Wabunge, Hassan Kaunje wa Lindi Mjini, Hassan Masala wa Nachingwea na Mbunge wa Liwale, Zuberi Kucheuka wamemuomba Rais John Magufuli awasaidie kushughulikia changamoto zilizo kwenye majimbo yao.

Wakizungumza katika ziara ya kikazi ya Rais huyo Mkoani Lindi leo Jumanne Oktoba 15, 2019, wabunge hao wamesema pamoja na jitihada mbalimbali za kutekeleza miradi ya kimaendeleo kwenye majimbo yao, bado yanakabiliwa na changamoto.

Mbunge wa Nachingwea, Masala amesema jimbo lake linakabiliwa na tatizo la migogoro ya ardhi, baadhi ya wakulima wa korosho wanalalamikia kutolipwa fedha zao na  ubovu wa barabara kutoka Nanganga – Rwangwa - Nachingwea mpaka Masasi.

“Kuna mgogoro mkubwa pale Majimaji kwenye kambi ya jeshi, wananchi wetu wanadai fidia kwa muda mrefu, jambo hili kwa namna lilivyobakia limebaki  kwako tu,” amesema Masala.

Kwa upande wake Mbunge, Kaunje amemuomba Rais Magufuli kusaidia kuwavuta wawekezaji kwenye jimbo hilo ili kuongeza ajira kwa wananchi wake.

Pia, ameiomba Serikali kujenga stendi na soko kwa sababu hawajaweza kujenga kutokana na uhaba wa fedha.

Mbunge wa Liwale, Zuberi Kucheuka ameomba kufunguliwa kwa barabara zinazo unganisha wilaya hiyo na nyingine.

Hata hivyo, amesema fedha zilizotolewa na Serikali mwaka jana zimesaidia kujenga vituo vya afya, miradi ya maji na maboma kwenye baadhi ya shule.

“Wana Liwale wamenituma niseme wamekuelewa, ulipoamua kutoa elimu  bure wamekuelewa wanasema wanakuunga mkono,” amesema Kucheuka.

Mwisho.