Wachina wa Baidu waiahidi makubwa Tanzania

Muktasari:

Wachina wa mtandao wa Baidu wameahidi kutumia picha za vivutio vya utalii vya Tanzania kuongeza idadi ya watalii kutoka taifa hilo

Dar es Salaam. Timu ya Wachina 11 kutoka mtandao wa Baidu waliokuja kupiga picha vivutio vya utalii wameahidi kutumia picha hizo kuitangaza Tanzania kupitia sekta ya utalii.

Wachina hao ambao walikuwa Tanzania kwa siku 11 wakiwa na kazi ya kupiga picha na video za vivutio kwa ajili ya kuviweka kwenye mtandao huo wa China unaofikiwa na watu zaidi ya 700 milioni.

Hilo limefanyika baada ya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi saba duniani zilizopo kwenye  mradi wa Wonder Planet unaotekelezwa na mtandao wa Baidu.

Akizungumza leo Jumapili Septemba 1, 2019 jijini Dar es Salaam kiongozi wa msafara huo, Hepburn Jin amesema wamejifunza vitu vingi kuhusu Tanzania ambavyo hawatavielezea katika mtandao huo pekee bali hata kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii.

Amesema kutokana na umbali uliopo kati ya China na Tanzania ni Wachina wachache wanaofahamu kuhusu Tanzania hivyo fursa hiyo wataitumia vyema kuwaeleza vilivyopo.

“Wakati nakuja nilijua Afrika ni bara lenye joto ila nimeona utofauti Tanzania kuna hali ya hewa nzuri, watu wakarimu, mandhari nzuri yote haya tutaenda kuyaelezea China,” amesema

Jin ameeleza picha na video walizochukua zitaanza kuwekwa kwenye mtandao huo katikati ya Septemba, 2019.

Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji mstaafu Thomas Mihayo amesema Tanzania kupata fursa ya kuelezewa kwenye Baidu ni hatua kubwa katika harakati za kuliteka soko la utalii la China.

“Tunaamini kwa idadi ya watumiaji wa mtandao huu hata tukiwapata watalii 100000 kutoka China itakuwa ni hatua nzuri, lengo ni kuliteka soko la utalii la nchi hiyo,” amesema Jaji Mihayo