Wachina watoa msaada kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko Lindi

Monday February 17 2020

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Dar es salaam. Kituo cha Kutoa huduma kwa Wachina wanaoishi Tanzania kimetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko mkoani Lindi vyenye thamani ya Sh30 milioni.

Vifaa hivyo ni nguo pea 6,000, blanketi 640, viatu pea 3,600, unga wa mahindi kilo 2,350 na madaftari ya 1,280.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu  Februari 17, 2020 jijini Dar es salaam mkurugenzi wa kituo hicho, Alston Yi amesema lengo ni kuwafariji wananchi hao.

"Tunatoa pole yetu kwa wananchi tunaamini ni mara kadhaa tumekuwa tukishiriki katika matukio ya kijamii, kwa hiyo msaada huu utakuwa sehemu ya faraja," amesema Yi.

Januari 27, 2020 wakazi wa vijiji sita vya wilaya ya Kilwa mkoani humo walikosa mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kubomoka na kujaa maji.

Kwa mujibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu hadi Februari 5, 2020 watu zaidi ya 15 wameripotiwa kufariki  na nyumba 1,746 kuharibiwa katika vijiji hivyo.

Advertisement

Akipokea msaada huo,  meneja wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa wa chama hicho, Jonston Weston amesema huduma nyingi bado zinahitajika kwa waathirika hao.

"Tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza katika suala hili, tunashukuru kwa msaada huu wa Wachina. Huu ni msaada wa tatu kutoka kwa wadau tuliopokea katika ofisi zetu, tumepokea kutoka kampuni ya Shell Tanzania pamoja na Shirika la Unicef,” amesema.

Hadi Februari 9, 2020 wananchi 843 walikuwa wamehifadhiwa katika kambi nne huku taasisi binafsi, mashirika, wafanyabiashara na viongozi wakitoa misaada.

Advertisement