Wadakwa wakidaiwa kuvuruga uandikishaji Serikali za mitaa

Friday October 11 2019Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa 

By Burhani Yakub, Mwananchi [email protected]

Tanga. Watu wanne wanashikiliwa na Polisi wakituhumiwa kuvuruga uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 baada ya kubainika kujiandikisha katika kituo zaidi ya kimoja.

Akizungumza leo Ijumaa Oktoba 11, 2019 mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa amesema watuhumiwa hao walikamatwa jana Alhamisi  katika vituo vya kata ya Ngamiani Kusini na Ngamiani Kati.

Amesema kwa sasa wanahojiwa na polisi, “wananchi wa Tanga msikubali kushawishiwa ili mfanye vurugu, ifahamike kwamba Serikali haiko tayari kuona zoezi hili linaingia dosari kwa namna yeyote.”

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi Wilaya ya Tanga, Ramadhani Posi amesema leo saa 6 mchana wakazi 44,615 wamejitokeza katika vituo 498 sawa na asilimia 34 ya wakazi 135,892  wanaotarajiwa kujiandikisha.

Advertisement