Wadau wa Kiswahili kuiteka Arusha kesho

Wednesday September 11 2019

By Gadi Solomon, Mwananchi [email protected]

Arusha. Kesho Alhamisi Septemba 12, 2019 jijini Arusha yatafanyika  maadhimisho ya kitaifa ya Kiswahili na utamaduni huku waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe akitarajiwa kuzindua kanuni za sheria ya kuanzishwa Baraza la Sanaa la Taifa (Bakita).

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Septemba 11, 2019 mkurugenzi wa Idara ya utamaduni wa wizara hiyo, Dk Emmanuel Temu amesema maadhimisho hayo ni  muhimu kwa Taifa kwa sababu hivi karibuni  lugha ya Kiswahili imepewa nafasi kuwa lugha ya nne katika nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).

Katibu mtendaji wa Bakita,  Dk Selemani Sewangi ametoa wito kwa wananchi kushiriki kongamano hilo, “Tukio hili ni  tofauti na  miaka mingine. Hii ni mara ya kwanza tunashirikiana na sekta binafsi.”

Katika kongamano hilo Bakita imeshirikiana na Chuo cha MS TDCD huku wageni kutoka nchi wanachama wa  Jumuiya ya Afrika Mashariki wakitarajiwa kushiriki wakiwemo mabalozi, walimu wa Kiswahili, wanafunzi, wahadhiri, wanahabari pamoja na wakuu wa  idara na taasisi za Kiswahili.

"Tangu chombo hiki kimeundwa kwa mara ya kwanza tutazindua kanuni za sheria," alisema  Dk Sewangi

Advertisement