VIDEO: Wadhamini wawasilisha maombi mahakamani ili Tundu Lissu akamatwe

Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu

Muktasari:

Lissu yupo Ubelgiji tangu Januari 6, 2018 alikokwenda kwa matibabu akitokea Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako nako alifikishwa usiku wa Septemba 7,  2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akiwa katika makazi yake eneo la Area D, Dodoma.

Dar es Salaam. Wadhamini wa aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu wamewasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutaka itoe kibali ili makamu mwenyekiti huyo wa Chadema akamatwe.

Desemba 19, 2019 Mahakama hiyo ilitoa amri kwa wadhamini hao kuhakikisha mshtakiwa huyo anafika mahakamani tarehe itakayopangwa.

Lissu ambaye kwa sasa yupo nchini Ubelgiji anakabiliwa na kesi ya uchochezi katika mahakama hiyo,  hakuonekana mahakamani Jumatatu ya Januari 20, 2020, huku wadhamini wakitakiwa na mahakama kuhakikisha anarejea nchini ili kuendelea na kesi yake.

Januari 30, 2020 Robert Katula ambaye ni mdhamini wa Lissu aliieleza mahakama hiyo kuwa juhudi walizofanya ni pamoja na kuwasiliana na mshtakiwa bila mafanikio pamoja na kumuandikia barua mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuwasaidia ili Lissu arejee nchini.

Akizungumza leo Alhamisi Februari 20, 2020 wakili wa Serikali mwandamizi,  Wankyo Saimon amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa lakini  wameshapokea nyaraka iliyowasilishwa mahakamani.

“Shauri hili limekuja kwa ajili ya kutajwa limekuwa likikwama kutokana na mshtakiwa wa nne kutokuwepo na leo tumepokea maombi namba mbili ya mwaka 2020 yaliyowasilishwa na wadhamini wakiiomba mahakama itoe kibali cha kumkamata mshtakiwa,” amedai wakili Wankyo na kuomba mahakama kupanga tarehe nyingine ili maombi hayo kusikilizwa.

Katula amedai wamefanya jitihada za kumleta Lissu lakini imeshindikana na kuomba mahakama itoe kibali cha kukamatwa, “ tumefanya jitihada za kumleta lakini imeshindikana tunaiomba mahakama itoe kibali cha kukamatwa ili tuweze kuwa huru na kufanya shughuli zetu.”

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 2, 2020 kwa ajili yakusikiliza maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wadhamini na kuangalia sheria inasemaje.

Katika kesi ya msingi Lissu na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mhariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na mchapishaji wa kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati  Januari 12 na 14, 2016 jijini Dar es Salaam ambapo Jabir, Mkina na Lissu waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi.