Wafanyabiashara Sao Hill kujibiwa Feb 17

Thursday January 30 2020
hill pic

Mkurugenzi wa Masoko na Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mohamed Kilongo akikagua msumeno wa kukatia magogo kwenye mojawapo wa viwanda vya mbao mjini Mafinga, mkoani Iringa.

Mafinga. Wadau wa shamba la miti la Sao Hill lililopo wilaya Mufindi mkoani Iringa wanahesabu siku kabla ya Serikali kuwaeleza hatua iliyofikia kutokana na malalamiko yao ya gharama za tozo wanazodai kuwa kubwa zinazowakwaza katika shughuli zao.

Akizungumza na wadau hao katika kikao maalumu kilichohusisha wafanyabiashara wa mazao ya msitu na wavunaji, naibu kamishna wa uhifadhi anayeshughulikia masoko na rasilimali za misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mohamed Kilongo aliwataka kuwa na subira ili kuzipa muda mamlaka za Serikali kuja na ufumbuzi wa malalamiko yao.

Kilongo aliwaambia kuwa ifikapo Februari 17, mwaka huu, TFS ambayo iko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wizara za Fedha, Viwanda na Biashara na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamsemi) watakaa ili kujadiliana juu ya malalamiko hayo.

Katika malalamiko ya wadau hao yaliyowasilishwa kwa Kilongo na baadhi ya wafanyabiashara waliopata fursa ya kuzungumza wakiongozwa na katibu wa Chama cha Wavunaji wa Misitu katika shamba hilo, Basil Tweve, walisema kumekuwapo na ongezeko la tozo ambazo zimesababisha wengine kufunga shughuli zao.

Tweve aliiomba Serikali kuangalia nama gani ya kupunguza tozo hizo ambazo zinaanzia halmashauri hadi Serikali kuu na hivyo kupunguza kipato wanachopata na wengine kuambulia hasara.

“Hili tunaomba lishughulikiwe maana baadhi ya wachamama wetu wameamua kufunga kabisa shughuli na wengine wanafanya tu ilmradi wapate faida kidogo, waweze kulinda mitaji yao,” alisema.

Advertisement

Mvunaji wa misitu, Chesko Ng’umbi alisema biashara imekuwa ngumu, na hivyo Serikali inapaswa kuwasaidia kuwatafutia masomo mapya ili waweze kuendelea na shughuli zao katika shamba hilo kubwa kuliko yote hapa nchini.

“Ukiangalia gharama za uvunaji ziko juu, tozo nazo zipo palepale na zingine zimekuja kuongezeka, lakini faida ni ndogo. Mimi nilikopa karibu Sh1.5 bilioni, lakini mtaji umekata nimeambulia Sh1.1 hivi, imekata karibu Sh300 milioni na ushee, nimebaki na deni kubwa,” alisema Ng’umbi.

Naye Mwachang’a Matekeleza aliiomba Serikali kuanzisha benki kwa ajili ya wafanyabiashara wa mazao ya misitu kama ilivyo kwa wakulima, lengo likiwa ni kuwarahisishia upatikanaji wa mikopo na urahisi wa kifedha katika uendeshaji wa shughuli zao.

“Tuletewe benki ya misitu ili tukope, vilevile huko shambani mtutengenezee vizuri barabara ili tunapokata miti hata wakati wa mvua usafirishaji wake uwe rahisi maana magari yetu huwa yanakwama na wakati mwingine kuharibika kutokana na barabara kutokuwa zingine mbovu,” alisema.

Grace Msina, mpasuaji wa mbao katika shamba hilo aliitaka Serikali kuyashughulikia haraka malalamiko yao ili yasije yakaathiri shughuli za uvunaji katika shamba hilo.

Akijibu hoja hizo na nyingine zilisowasilishwa kwake, Kilongo aliwataka wadau hao kuvuta subira na kwamba, kila hoja itajibiwa ifikapo siku hiyo.

Hata hivyo aliwataka waliomaliza uvunaji kuwasiliasha maombi mapya haraka ili wapatiwe vibali vipya.

Awali, mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri William aliwataka wafanyabiashara wa mbao wenye malalamiko ya tozo kuziwasilisha kwa mamlaka husika ikiwamo ile ya Mapato (TRA) ili zipatiwe ufumbuzi.

“Katika hili (la baadhi ya wafanyabiashara hao kufunga viwanda vya upasuaji wa mbao kwa madai ya kodi), linazungumzika waende tu TRA wakazungumze maana hata Serikali imekwishasema hakuna biashara itakayofungwa kwa sababu ya kodi, hivyo watapata ufumbuzi, wasiogope hii ni Serikali yao,” alisema William.

 

Advertisement