Wafanyabiashara mazao ya misitu kizimbani kwa uhujumu uchumi

Muktasari:

Wafanyabiashara wanne wa mazao ya misitu nchini Tanzania wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji wa Sh155 milioni.


Dar es Salaam. Wafanyabiashara wanne wa mazao ya misitu nchini Tanzania wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji wa Sh155 milioni.

Wafanyabiashara hao ni mkurugenzi mwendeshaji wa kampuni ya Allvay Product Farm, Ebenezer Mmanyi; Jumanne Brashi; Manish Khattar  na Rajesh Velram.

Kwa nyakati tofauti wamesomewa mashtaka  yao leo Jumatano Januari 29, 2020.

Mmanyi amesomewa mashtaka 10 na wakili wa Serikali mwandamizi, Ladislaus Komanya mbele ya Hakimu Mkazi, Vicky Mwaikambo.

Miongoni mwa mashtaka aliyosomewa Mmanyi ni kuongoza genge la uhalifu, akidaiwa kati ya Oktoba Mosi  na 31, 2015 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam akiwa na wenzake ambao hawakuwepo mahakamani waliongoza genge la uhalifu.

Mmanyi anakabiliwa na  kosa la kusafirisha mazao ya misitu kosa analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi na Oktoba 31, 2015 katika maeneo ya Dar es Salaam.

Anadaiwa alisafirisha mazao ya Sh6 milioni kwa kutumia kontena huku akijua kuwa hana kibali.

Kosa jingine ni utakatishaji  wa Sh6.5 milioni, analodaiwa kulifanya Oktoba 31, 2015 wakati akijua fedha hizo ni zao la makosa tangulizi.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashtaka yanayomkabili.

Brashi amesomewa mashtaka na wakili wa Serikali, Tuli Helela mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rashidi Chaungu.

Helela amedai kati ya Januari Mosi, 2015 na Oktoba 31, 2015 mshtakiwa akiwa na watu wengine ambao hawakuwepo mahakamani waliongoza genge la uhalifu.

Wakili Helela amedai  katika shitaka jingine la  usafirishaji haramu wa mazao ya misitu, anadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2015 na Oktoba 31, 2015 alisafirisha mazao ya misitu yaliyokuwa kwenye kontena tano za magogo ya Sh32.6 milioni bila kuwa na kibali kutoka kwa mamlaka husika.

Katika shitaka la tisa la ukwepaji kodi, Helela amedai siku hiyo, mshtakiwa aliwasilisha nyaraka za uongo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa nia ya kukwepa kodi ya Sh32.6.milioni

Katika shtaka la mwisho la utakatishaji fedha,  inadaiwa kati ya Januari 2015 na Oktoba 31, 2015 mshtakiwa alijipatia Sh32,630,000 wakati akijua fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la ukwepaji kodi.

Baada ya kusoma hati ya mashtaka, Helela amedai upelelezi wa shauri hilo bado  haujakamilika na kuomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine huku Brashi akipelekwa rumande.

Washtakiwa Khattar na Velram wamesomewa mashtaka yao na wakili wa Serikali, Elizabeth Mkunde na Silivia Mitanto mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega.

Wawili hao wanakabiliwa na makosa saba, likiwemo la  kughushi kusafirisha mazao ya misitu, kushindwa kulipa kodi na utakatishaji fedha.

Katika kosa la utakatishaji fedha, wanadaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi na Oktoba, 2015 kati ya Tanzania na Zambia.

Wanadaiwa kutakatisha Sh117.48 milioni ikiwa ni mali ya Serikali ya Tanzania huku wakijua zimepatikana  kwa makosa tangulizi.

Kesi hizo zimeahirishwa hadi Februari 12, 2020 zitakapokuja kwa ajili ya kutajwa.