Wafanyakazi benki ya Akiba wahukumiwa kulipa faini, fidia ya Sh62 milioni

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu  wafanyakazi wanne wa Benki ya Akiba tawi la Ilala kulipa fidia ya Sh62 milioni baada ya kukiri kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu  wafanyakazi wanne wa Benki ya Akiba tawi la Ilala kulipa fidia ya Sh62 milioni baada ya kukiri kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Pia mahakama hiyo imewahukumu kulipa faini ya Sh200, 000 kila mmoja na wakishindwa watumikie kifungo cha mwaka mmoja gerezani.

Washtakiwa hao ni Frank Kihedu, Wahenda Ally, Abdilla Amanzi na Isabela Ladislaus.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu Machi 30, 2020  na Hakimu Mkazi  wa mahakama hiyo, Rashid Chaungu.

Chaungu amesema kwa kuwa washtakiwa hao wamekubali kosa mahakama inawahukumu kulipa faini ya Sh200,000 au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani .

Chaungu alisema pia makubaliano mliyoingia na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) yatekelezwe kwa kufidia hasara waliyosababisha na kutakiwa kulipa Sh62 milioni.

Katika kesi hiyo kati ya  Juni Mosi 2013 na Oktoba 24, 2013 washtakiwa wakiwa maeneo ya benki ya Akiba tawi la Ilala jijini Dar es Salaam kwa nia ya kufanya udanganyifu kwa makusudi walijipatia Sh62 milioni kwa kudanganya kwamba walielekezwa kutoa fedha kwenye akaunti mbalimbali za wateja wa benki hiyo wakati wakijua si kweli.