Wafanyakazi wa Serikali wafurika kuomba kustaafu kwa hiari

Katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi wa taasisi ya Elimu ya juu,Sayansi,Technolojia,ufundi stadium,Habari na Utafiti, Winston Makere akizungumza katika semina ya viongozi wa RAAWU nchini jijini Arusha.

Muktasari:

Idadi ya wafanyakazi ambao wanaomba kuacha kazi kwa hiari imeongezeka ili kulipwa mafao yao kabla ya 2023

Arusha. Kumekuwapo na ongezeko kubwa la wafanyakazi wa Serikali, kuomba kustaafu kwa hiari ili kulipwa mafao kwa kikokotoo cha sasa ambacho kitafikia ukomo mwaka 2023.

Katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia Ufundi Stadi, Ushauri, habari na Utafiti (RAAWU) , Winston Makere  ametoa taarifa hiyo leo, Jumatatu Septemba 16 wakati anafungua semina ya viongozi wa RAAWU nchini.

Amesema kutokana na ongezeko kubwa la watumishi kutaka kustaafu kwa hiari kabla ya miaka yao, hivi sasa wizara ya Utumishi, imeanza kusita kupokea maombi ya watu kustaafu kwa hiari.

" Ndio sababu bado tunaomba suala hili, tuendelee na majadiliano, awali tulipendekeza malipo ya mkopo yabaki asilimia 50 lakini Serikali ikapinga, tukapendekeza asilimia 40 pia ikakataliwa na sasa tunajadliana malipo ya asilimia 37.5,"amesema.

Amesema chama hicho kwa kushirikiana na shirikisho la vyama vya wafanyakazi, pia bado wanaomba pungufu ya kodi katika mishahara ya wafanyakazi wote kwani wanalipa kodi kubwa kuliko hata wafanyabiashara.

“Serikali ilitangaza kuondoa kodi kwa mishahara kima cha chini Sh 170,000 na wengine wenye mishahara ya kati na mikubwa  bado wanalipa kodi kubwa tunaomba pungufu,”amesema.