Wafuasi wa Chadema, ACT-Wazalendo kortini Kilimanjaro

Muktasari:

  • Watano wameshitakiwa kwa madai ya kuchoma ofisi ya Serikali na mmoja na wenzake wanne ambao wanatafutwa kwa madai ya  kumpora msimamizi msaidizi wa uchaguzi

Moshi. Watu sita wanaoaminika ni wafuasi wa vyama vya upinzani vya Chadema na ACT- Wazalendo, wamefikishwa mahakamani katika kesi mbili tofauti jana Jumatatu Novemba 11,2019 ikiwamo ya kuchoma ofisi ya mtendaji wa kata ya Soweto katika Manispaa ya Moshi.

Katibu wa Chadema mkoa Kilimanjaro, Basil Lema alithibitisha watuhumiwa watano kati ya sita ni wafuasi wao na mmoja ambaye hakumtaja kwa jina ni mwanachama wa chama cha ACT- Wazalendo.

Hata hivyo, hati ya mashitaka iliyosomwa mahakamani na mawakili wa Serikali kutoka Divisheni ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Kassim Nassir na Ignas Mwinuka haikuwataja watuhumiwa kama wafuasi wa vyama hivyo vya siasa.

Waliofikishwa mbele ya Hakimu mkazi Moshi, Jullieth Mawolle kwa kuchoma ofisi ya Afisa mtendaji wa Kata ya Soweto ni pamoja na Diwani wa Kata hiyo kwa tiketi ya Chadema, Collins Mayuta (40), ambaye pamoja na wenzake wanne walikana mashitaka dhidi yao.

Watuhumiwa wengine ni Mohamed Bakari(27), Paulo Lyimo(37), Priscus Kayanda (44) na Juma Ally (27), ambao hawakuweza kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini watakaosaini bondi ya Sh2 milioni isipikuwa Mayuta pekee aliweza kudhaminiwa.

 

Wakili Nassir alidai Novemba 10, 2019 huko mtaa wa Wales eneo la Soweto, bila uhalali wowote, watuhumiwa wote waliwasha moto katika ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata ya Soweto huku wakijua kufanya hivyo ni kosa.

Katika shitaka la pili, Wakili Nassir alidai siku hiyo hiyo, bila uhalali wowote  washitakiwa hao walifanya uharibu wa samani za ofisi za ofisi ya Afisa mtendaji wa Kata ya Soweto zenye thamani ya Sh1.3 mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Washitakiwa hao pia wameshitakiwa kwamba siku hiyo pia waliisababishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasara ya Sh1.3 milioni kutokana na matendo yao yasiyo halali ya kuwasha moto ofisi ya mtendaji Soweto.

Washitakiwa wote walikanusha mashitaka hayo na kutakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja watakaosaini dhamana ya Sh2 milioni, ambapo hata hivyo ni Mayuta tu aliweza kuyatimiza na kesi kesho Novemba 12  kwa ajili ya kushughulikia dhamana kwa washitakiwa wanne.

Katika hatua nyingine, mtuhumiwa mwingine anayedaiwa kuwa mfuasi wa Chadema wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Godwin Mushi jana alifikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi akikabiliwa na mashitaka ya unyang'anyi wa kutumia silaha.

Mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi, Pamela Mazengo na kusomewa shitaka lake na wakili wa Serikali kutoka NPS, Ignas Mwinuka na kukanusha mashitaka hayo na kupelekwa gereza la Karanga kwa kuwa shitaka hilo halina dhamana.

Wakili Mwinuka alidai kuwa Novemba 4,2019 katika ofisi ya kijiji cha Mamba wilaya ya Hai, mtuhumiwa pamoja na wenzake wanne ambao bado hawajakamatwa walimpora vitu na fedha, Tegemea Massawe ambaye ni msimamizi msaidizi wa uchaguzi katika eneo hilo.

Ilidaiwa kuwa siku hiyo, washitakiwa walimpora Massawe simu aina ya Techno yenye thamani ya Sh400,000, simu aina ya Nokia yenye thamani ya Sh150,000 na fedha taslimu Sh390,000 ambapo kabla au baada ya uporaji huo walimshambulia Massawe kwa mawe na fimbo.

Kesi hiyo imepangwa kutajwa Novemba 22,2019.