Wafungwa 207 waachiwa Manyara

Baadhi ya wafungwa waliokuwa gereza la Mrara Mjini Babati Mkoani Manyara, walioachiwa leo kwa msamaha wa Rais John Magufuli. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Wafungwa hao ni kati ya 5,533 walioachiwa kwa msamaha wa Rais John Magufuli alioutoa jana katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika

Babati. Wafungwa 207 mkoani Manyara leo Jumanne Desemba 10, 2019 wameachiwa huru.

Wafungwa hao ni kati ya 5,533 walioachiwa kwa msamaha wa Rais John Magufuli alioutoa jana katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika.

Akizungumza na wafungwa hao mjini Babati mkuu wa Mkoa wa Manyara,  Alexander Mnyeti amewataka watumie fursa hiyo kuwa wema na wakifika uraiani wasirudie makosa yao.

"Mmepewa msamaha na Rais Magufuli jana sasa sitarajii kusikia kesho kutwa mmerudishwa tena magereza kwa kufanya makosa, mkifika uraiani muwe watu wema na siyo kufanya uhalifu kwa mara nyingine," amesema.

Ofisa magereza wa mkoa wa Manyara, Lipina Lyimo amesema kati ya wafungwa hao, 141 walikuwa gereza la Mrara mjini Babati, 21 gereza la Kiteto na 45 wa gereza la Wilaya ya Mbulu.

Amesema walioachiwa huru ni waliokuwa na makosa madogo na waliobakiza siku chache kumaliza vifungo vyao, kuanzia siku moja hadi miezi 12.