Wafungwa 74 waliotoka gerezani kwa msamaha wa Magufuli wapewa mashamba

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera

Katavi. Wafungwa 74 katika Mkoa wa Katavi waliotoka gerezani kwa msamaha wa Rais wa Tanzania, John Magufuli wamepewa ekari 370 za ardhi  kwa ajili ya kilimo.

Akizungumza leo Jumanne Desemba 10, 2019 mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera amesema kila mmoja atapata ekari 5 kwa ajili ya kilimo.

"Najua wengine mtakuta wake zenu wameolewa, nendeni  mkaoe tena, nawapa   maeneo hayo mkalime msirudie kutenda  makosa, mtarudishwa tena gerezani," amesema Homera.

Augustino Maico, mkazi wa Inyonga Halmashauri ya Mlele ambaye alikamatwa na bangi ameshukuru kwa msamaha huo akibainisha kuwa amejifunza mambo mengi alipokuwa gerezani.

"Namshukuru mkuu wa Mkoa kutupa ekari 5 zitatusaidia katika kilimo, gerezani sio sehemu ya kufanya kitu unachojisikia kwa uhuru, lakini ni chuo tumejifunza tabia na vitu vingi," amesema Maico.

Juma Maulid (19) aliyefungwa kwa kosa la kuiba pikipiki amesema maisha ya gerezani yamemsaidia kuongeza nguvu za kufanya shughuli mbalimbali.

"Nimeishi gerezani siku 19, niliiba pikipiki nimejifunza namna ya kulala ukiwa gerezani, wakati nikiwa uraiani nilikuwa sina nguvu za kulima, lakini kwa sasa nina nguvu nyingi  nikazitumie kulima," alisema Maulid.

Kati ya wafungwa hao 74, wafungwa 43 ni wa gereza la Mpanda na 31 gereza la  Kalilankulukulu.