Wagombea upinzani ambao hawakujitoa uchaguzi Serikali za mitaa kupigiwa kura kesho

Muktasari:

Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo amesema wagombea ambao hawakuandika barua ya kujitoa uchaguzi wa Serikali za mitaa na vyama vyao havikufuata mchakato wa kujitoa, majina yao hayataondolewa.


Dodoma. Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo amesema wagombea ambao hawakuandika barua ya kujitoa uchaguzi wa Serikali za mitaa na vyama vyao havikufuata mchakato wa kujitoa, majina yao hayataondolewa.

Ametoa maelezo hayo leo Jumamosi Novemba 24, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma kuzungumzia uchaguzi huo unaofanyika kesho Jumapili Novemba 24, 2019.

Vyama vilivyojitoa katika uchaguzi huo ni NCCR-Mageuzi, Chadema, UPDP, CUF na ACT-Wazalendo.

Jafo amesema  vyama vya siasa vilivyoandika barua za kujitoa katika uchaguzi huo na kutimiza vigezo vya kujitoa, majina ya wagombea wao hayatakuwepo.

Hata hivyo, amesema suala la kujitoa lilikuwa la hiari na kwamba baadhi ya vyama vilijitoa ngazi ya juu lakini wagombea wake hawakujitoa.

“Baada ya kutangaza kujitoa nilitoa maelekezo kwa vyama kwa mujibu wa ibara ya 19 na 20 ya kanuni za uchaguzi kuwa wagombea walipaswa kuandika barua za kujitoa sasa kama hawakufanya hivyo watakuwa ni wagombea," amesema Jafo.