Wagonjwa wa corona Tanzania wafikia watatu

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imetangaza wagonjwa wawili zaidi wenye virusi vya corona leo Jumatano, Machi 18, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema baada ya kuchukuliwa sampuli za wagonjwa hao mmoja ambao walipatikana Zanzibar na mmoja Dar es Salaam.
“Tuna mgonjwa mmoja kutoka Zanzibar ambaye sampuli zake zililetwa maabara kuu ni mjerumani (24) amepata maambukizi yupo kwenye uangalizi, lakini pia hapa jijini Dar es Salaam na mmarekani mwenye miaka 61 naye amegundulika kuwa na virusi vya corona,” amesema Majaliwa.
Katika hatua nyingine, Majaliwa amesitisha masomo ya vyuo vikuu na kati na vyuo ambavyo wanafunzi wako likizo wametakiwa kubakia nyumbani.
“Wale wachache ambao wanamalizia mitihani wakimaliza waondoke mara moja ili kuondoa misongamano na vyuo vya kati vya ufundi na ualimu waliotakiwa kufanya mtihani Mei mwaka huu namuagiza Waziri wa Elimu afanye marekebisho ya mihula ya elimu kama ya kidato cha sita.”
Majaliwa amewataka Watanzania kuendelea na shughuli za kila siku na taarifa zitazidi kutolewa na shughuli mbalimbali zitaendelea kusitishwa kutokana na hali itakavyokua.
Amesisitiza kutofanya misongamano na mikusanyiko isiyo na umuhimu huku shughuli za masoko na maduka zitaendelea.
“Huduma za usafirishaji zitaendelea lakini wasafirishaji waendelee kuwaelimisha abiria hakuna umuhimu wa kujaza watu wakikaa kwenye viti gari iende.
Serikali imesema inaendelea kuwahifadhi wagonjwa hadi ugonjwa huo utakapoisha na hatua zinaendelea kuchukuliwa katika mipaka na sehemu za uingiaji wageni