VIDEO: Wagonjwa wa corona Tanzania wafikia 19

Muktasari:

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema wagonjwa wa corona nchini Tanzania wamefikia 19, baada ya watano kuongezeka leo Jumatatu Machi 30, 2020.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema wagonjwa wa corona nchini Tanzania wamefikia 19, baada ya watano kuongezeka leo Jumatatu Machi 30, 2020.

Taarifa iliyotolewa na waziri huyo leo inaeleza kuwa wagonjwa hao watano walifanyiwa vipimo katika maabara kuu ya Taifa, “kati ya wagonjwa hawa, watatu ni kutoka Dar es Salaam na wawili kutoka Zanzibar ambao taarifa zao zimetolewa na Waziri wa Afya Zanzibar.”

“Hivyo sasa jumla ya wagonjwa wa corona ni 19 akiwemo mgonjwa mmoja aliyetolewa taarifa na Waziri wa Afya Zanzibar Machi 28, 2020.”

Kuhusu taarifa za wagonjwa wapya wa Dar es Salaam, Ummy amesema, “mwanaume mwenye miaka 29 Mtanzania alikutana na raia wa kigeni kutoka miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi. Mwanamke mwenye miaka 21 Mtanzania ambaye ni miongoni mwa watu waliokuwa wakifuatiliwa.”

“Mwanaume mwenye umri wa miaka 49 Mtanzania ambaye pia ni miongoni mwa watu waliokuwa wakifuatiliwa.”

Taarifa hiyo inaeleza kuwa kazi ya kufuatilia watu wote wa karibu waliokutana na wagonjwa hao inaendelea, kuwataka watu kuendelea kuchukua tahadhari ili kujikinga na ugonjwa huo ambao hadi leo saa 7:00 mchana, watu zaidi ya 30,000 wameripotiwa kufariki kwa ugonjwa huo.