Wagonjwa wa mguu Kifundo wanvyorejeshewa tabasamu na Tigo

Dar es Salaam. Siku zote ni furaha pale mwanamke anapopata mtoto ambaye alimtarajia baada ya miezi tisa ya ujauzito. Hii ilidhihirika kwa Salma Hajj (29) baada ya kujifungua salama mtoto wake wa kwanza wa kiume miezi 10 iliyopita.

Hata hivyo, furaha ya Salma haikudumu.Baada ya muda mfupi, Salma ambaye ni mkazi wa Buza jijini Dar es Salaam aligundua kuwa mwanae huyo alikuwa na tatizo la miguu kujikunja pasipo kujua ni nini tatizo.

Tatizo hilo linajulikana kama ‘mguu kifundo’ au kwa kiingereza linafahamika kama ‘Clubfoot’ ambalo kisayansi linalotokea hata kabla ya mtoto kuzaliwa.

Kila mwaka zaidi ya watoto 100,000 duniani huzaliwa na ugonjwa huu ambao humfanya mtoto kushindwa kutembea kwa kutumia unyayo na badala yake hutumia kifundo cha mguu.

Kwa Tanzania,inakadiriwa kuwa karibuni watoto 2,800 wanazaliwa na ugonjwa huu kila mwaka.Kati yao asilimia 50 wana athirika mguu mmoja huku waliobaki wakiathirwa miguu yote miwili.

Asilimia 80 ya wagonjwa wasiopata matibabu yake wanapatikana kwenye nchi zinazoendelea, ikiwamo Tanzania.Kama ugonjwa huu usipotibika unaweza kusababisha maumivu makali wakati wa kutembea na hatimaye husababisha ulemavu wa muda mrefu.

 “Kiukweli ulikuwa ni wakati mgumu sana kwangu.Nilijisikia vibaya kwamba mwanangu hataweza kutembea vizuri na hatahivyo sikujua anasumbuliwa na tatizo gani,” anasema Salma.

Anaongeza: Nilihisi kama ilikuwa mwisho wa dunia kwangu na mwanangu; nilijiuliza maswali mengi bila majibu kwamba atawezaje kutembea?  ataonekanaje kwa watu? atasoma katika shule gani? nilichanganyikiwa sana.

Wakati bado anahaha kutafuta msaada, mmoja wa wauguzi alimjulisha kuwa tatizo hilo linaweza kutibika katika Hospitali ya CCBRT iliyoko Msasani jijini Dar es Salaam bila malipo. Kilichofuata ilikuwa ni kutembelea hospitalini hapo ambapo madaktari walianza kutoa matibabu kwa mtoto wake.

Kwa mujibu wa daktari wa mifupa (Orthopedic) wa CCBRT, Dk. Zainab Ilonga, chanzo cha ugonjwa huo bado hakijulikani.

Anasema hadi sasa sababu yake bado haijathibitika lakini wanaamini  ni matumizi ya pombe na matumizi mabaya ya madawa wakati wa ujazuzito au urithi wa vinasaba (genetic) na kwamba tafiti zaidi zitasaidia kutambua chanzo halisi cha tatizo hilo.

 “Kuna njia mbili za kutibu ugonjwa huu wa mguu kifundo;moja ni kutumia njia ya Ponseti ambayo haihitaji kufanya upasuaji na nyingine ya kufanya upasuaji,” Dk Ilonga anasema na kuongeza 

Kwa Tanzania  watoto 400 wanatibiwa kwa mwaka sawa na asilimia 25 ya wagonjwa wote na hii inatokana na baadhi ya wazazi kuwanawaficha watoto wenye tatizo hili.”

 

Ignacio V. Ponseti ni njia ambayo imekuwa ikitumia kutibu mguu kifundo tangu miaka ya 1940.Moja ya kanuni ya njia hii ni kwamba tishu za mtoto ikiwamo tendoni, ligamenti na maungio yake yapo katika hatua ya ukuaji hivyo kufanya mguu kuungana baada ya kila wiki moja.

Kwa kutumia njia hii ndani ya wiki kadhaa hali ya mgonjwa inaweza kubadilika na kufanikisha kurekebisha mguu bila uhitaji wa kufanya upasuaji.

Mtoto wa Salma alipitia hatua hiyo maarufu kama ‘gentle bone manipulations’ na ufuatiliaji (castings) ili kujua mabadiliko ya kibaolojia hasa misuli yake, maungio na tishu kwa lengo la kutibu tatizo alilokuwa nalo. 

“Kuna wakati alikuwa anapitia wakati mgumu kwani alikuwa analia sana jambo lililonifanya na mimi kulia.Nilikuwa na wasiwasi juu ya maisha ya mwanangu siku za mbeleni,” anasema kwa huzuni.

 “Nawashukuru sana Tigo na madaktari  wa CCBRT kwa msaada wao mkubwa kwasababu mtoto wangu ana miezi kumi kwa sasa na amepona kabisa,” anasema Salma huku akitabasamu.

Afisa wa Uwajibikaji kwa Jamii wa Tigo, Halima Okash anasema waliona  umuhimu wa kusaidia wahitaji kwasabau CCBRT inahudumia jamii yenye uhitaji na wasiojiweza katika kuwasaidia kupata huduma za matibabu.

“Tumeunga mkono jitihada hizi zinazofanywa na CCBRT kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata nafasi ya kutibiwa kwa gharama ndogo au bure kabisa,” anasema Okash.

Kupitia huduma za upasuaji kutoka hospitali ya CCBRT jumla ya watoto 1,509 wamenufaika katika kipindi cha miaka sita iliyopita. 

“Haya ni mafanikio yanayotufanya sisi Tigo kujisikia faraja kwa kiasi kikubwa kwani kwa  kutoa matibabu kwa watu wenye ulemavu,Tigo na CCBRT tunaleta matokeo chanya kwa maisha ya mtu mmoja mmoja, familia na jamii ya Tanzania kwa ujumla,” anasema Okash.

Tangu mwaka 2013, Tigo iliingia ubia na hospitali ya CCBRT kutoa matibabu kwa wagonjwa wa midomo sungura, kwa kutumia njia ya SMS zinazotumwa kwa wagonjwa wa CCBRT kuwakumumbusha kufuatilia matibabu na kutoa uelewa kuhusu huduma kwa umma.

Kupitia mpango huu, wagonjwa wanaweza kupata jumbe za matibabu kwa siku nne na siku moja kabla ya siku ya matibabu na hii imeisaidia CCBRT kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokatisha matibabu.

Kwa msaada wa Sh110 milioni kwa mwaka kutoka Tigo, CCBRT inaweza kutoa huduma za matibabu kwa njia Ponseti (bila upasuaji) kwa wagonjwa wapya zaidi ya 400 na wengine wanaoendelea na matibabu hospitalini hapo.