Wagonjwa wawili wa corona waongezeka Zanzibar

Waziri Afya Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed

Dar es Salaam. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetangaza uwepo wa wagonjwa wawili wapya wenye maambukizi ya virusi vya corona visiwani humo na sasa jumla wamefikia saba.

Taarifa ya Waziri Afya Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed imeeleza kuwa wagonjwa hao ni raia wa Tanzania ambao kwa nyakati tofauti waliingia visiwani Zanzibar kutokea mkoani Tanga.

Mohamed amesema watu hao waliingia kupitia bandari ya Mkokotoni mmoja ni mwanaume mwalimu wa shule wa mkoani Tanga aliingia Machi 18 na mwingine ni mfanyakazi wa hoteli (27) alienda Tanga Februari na kurudi Machi 13.

“Wagonjwa wote wanaendelea na matibabu katika kituo cha matibabu ya corona cha Kidimni na hali zao zinaendelea vizuri” imeeleza taarifa ya Mohamed

Serikali ya Zanzibar imetoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari zote zinazotolewa na wataalamu wa afya ikiwemo  kunawa mikono kwa sabuni, kuepuka mikusanyiko na kuepuka mambo yote yanayopelekea maambukizi.