UCHAGUZI MKUU 2020: Wagonjwa wodini walibebwa kwenda kupiga kura uchaguzi mkuu wa 1970

Tanzania ilifanya uchaguzi wake wa kwanza chini ya mfumo wa chama kimoja mwaka 1965 na kutokana na watu kutojitokeza kwa wingi kupiga kura mwaka 1970 kulikuwa na jitihada za ziada.

Wagonjwa waliokuwa wamelazwa hospitali walitakiwa kwenda kupiga kura.

Ilikuwa ni miaka mitano baada ya Katiba ya jamhuri ya Muungano kufanyiwa marekebisho yaliyoondoa siasa za vyama vingi.

Uchaguzi huo mkuu ulifanyika Oktoba 30 na waliojiandikisha kupiga kura za kumchagua Rais na wabunge walikuwa watu milioni 5.05. Hata hivyo, waliojitokeza kupiga kura walikuwa milioni 3.64, sawa na asilimia 72.2.

Mgombea pekee wa kiti cha urais aliyepitishwa na vyama vya Tanu na Afro-Shiraz alikuwa Mwalimu Julius Nyerere ambaye alipata kura milioni 3.575 za “Ndiyo”, ikiwa ni sawa na asilimia 96.93. Kura za “Hapana”, yaani zilizomkataa, zilikuwa 109,828, ambayo ni sawa na asilimia 3.07.

Nyerere alikuwa miongoni mwa wapigakura wa mwanzo kabisa kupanga foleni katika kituo cha Kijitonyama. Akiwa katika foleni, Nyerere alimpisha mpigakura ambaye alikuwa na dharura ya kufiwa na nduguye siku hiyo alfajiri. Mtu huyo alipiga kura kisha kuondoka kwenda kuzika.

Matokeo ya uchaguzi huo yalitangazwa na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi iliyokuwa iliyoongozwa na Y. Osman katika ukumbi wa Diamond mjini Dar es Salaam.

Sehemu mbalimbali za mji zilikuwa na magari yaliyokuwa yakifanya kazi ya kubeba wagonjwa kuwapeleka vituo vya kupiga kura kwa ajili ya kutimiza haki hiyo muhimu. Miongoni mwao alikuwepo mwanamke aliyepelekwa kituo cha kupiga kura cha Mburahati kwa kutumia gari la mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Dar es Salaam.

Katika uchaguzi huo mawaziri wawili, mawaziri wadogo saba pamoja na wabunge 40 walishindwa.

Isaak Bhoke Munamka, mmoja wa wanachama wa mwanzo kabisa wa Tanu waliojiunga na chama hicho mwaka 1954, alitetea kiti chake cha Tarime alichoshinda mwaka 1965. Lakini alishindwa na Aelius Gallus Omolo aliyepata kura 10,369 dhidi ya kura 9,524 za Munamka. Jumla ya kura 2,813 ziliharibika.

Munamka aliyezaliwa mwaka 1927 Mara Kaskazini na kupata elimu yake ya sekondari mkoani Tabora, alianza kazi kama karani wa serikali na kuonyesha utashi wa siasa mapema alipo na Chama cha Watanganyika ambako baadaye alikuwa makamu wa rais.

Alijiunga na Tanu wakati ikiundwa mwaka 1954 na akajijengea heshima kama mwanasiasa machachari akiusumbua utawala wa kikoloni.

Baadaye aliteuliwa kuwa mweka hazina wa chama hicho mwaka 1958. Mwaka huo alijaribu kumshawishi Nyerere asigombee katika uchaguzi wa mwaka 1958 kutokana na kutokuwa wa haki, lakini hakufanikiwa na Munanka akaingia katika uchaguzi na kushinda kiti cha Mara Kaskazini.

Baadaye akawa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais hadi Juni, 1965 alipohamishiwa Wizara ya Nchi, Tawala za Mikoa akiwa na jukumu la kusimamia serikali katika ngazi ya chini.

Lakini alishindwa kujenga ushawishi kwa wapigakura na mwaka 1970 wakati wananchi walipokuwa huru kuchagua wanayemtaka, alishindwa. Munamka anajulikana kutokana na taarifa kwamba alikataa kuonyesha sehemu aliyekuwepo Mwalimu Nyerere wakati wa uasi wa wanajeshi mwaka 1964, licha ya kutishiwa bunduki. Pengine kutokana na jambo hilo, Nyerere alimteua kuwa msaidizi wake binafsi baada ya kushindw auchaguzi.

Munamka hakupendwa na serikali ya kikoloni ambayo ilifunga matawi ya chama wilayani kwake na kumfunga jela.

Uchaguzi huo pia ulimuhusisha Ibrahim Haruna Lipumba, ambaye aligombea kwa alama ya nyumba katika Jimbo la Urambo ambako alipata 6,026. Hata hivyo, kura zake hazikutosha kumzidi mpinzani wake Said Ali Maswanya aliyepata kura 14,902.

Mwingine aliyeanguka ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mjini, J. W. Kihampa, pamoja na Waziri Mdogo katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Francis Vincent Mponji, walikuwa wa kwanza kutangazwa kushindwa vibaya katika uchaguzi huo.

Kihampa aligombea Jimbo la Bwakirwa ambako alipata kura 7,656 wakati mpinzani wake, Issa Kiyombwe alikusanya kura 18,698. Katika jimbo hilo kulikuwa na kura 383 tu zilizoharibika.

Mponji, ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa 1965 alipita bila kupingwa, alipata kura 5,862 wakati mshindi wa kiti hicho cha Nanyumbu alipata kura 26,563.

Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Amir Jamal, alipata kura 22,570 katika Jimbo la Morogoro baada ya kumshinda Ali Magara, aliyepata kura10,270.

Wakati matokeo yakiendelea kutangazwa, Tatu Mandara ambaye aligombea jimbo la Dar es Salaam Mashariki na kushindwa na Salehe Abdulla Yahya, alifungua kesi Mahakama Kuu kupinga ushindi huo. Tatu alishindwa kwa kura 1,339.

Mkoani Arusha, Joel Solomoni Kivuyo, ambaye alikuwa akitumia alama ya nyumba katika karatasi ya kupigia kura, alimshinda aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Obedi Ole Mejooli aliyekuwa akitumia alama ya jembe. Kivuyo alipata kura 19,353 dhidi ya 17,331 za Mejooli.

Patrick Silverius Quorro alipata kura 11,986 dhidi ya kura 11,630 za mpinzani wake, Merrus Richard Merrus. Katika jimbo la Mbulu mshindi alikuwa Damian Buya Geay aliyepata kura 16,022 dhidi ya Leandry Gobre Bilauri (3,839).

Katika jimbo la Meru, Jafet Ngura Kiliro alipata kura kura 14,899 dhidi ya Salome Ninyiti Filemoni (23,411) na Dar es Salaam Kusini aliyeshinda alikuwa Kitwana Selemani Kondo (41,325) dhidi ya Hassan Athumani Kilima (17,914). Kitwana Kondo alikuwa mbunge katika bunge lililotangulia kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 1970.

Dar es Salaam Kaskazini ushindi ulikwenda kwa Derek Bryceson (alama ya jembe) aliyepata ushindi wa kura 40,572 baada ya kupata kura 50,117 dhidi ya Aloys Henjewele (alama ya nyumba) aliyepata kura 9,545. Kura zilizoharibika ni 913.

Dar es Salaam Mashariki wagombea walikuwa ni Saleh A. Yahya (alama ya jembe) na Tatu Nuru Mandara (alama ya nyumba). Yahya alishinda kwa kura 1,339 baada ya kupata kura 20,377 dhidi ya kura 19,038 za Mandara.

Pare Kaskazini Peter Abdallah Kisumo (alama ya jembe) alimshinda Simeon Manase Kijo kwa kura (alama ya nyumba) kwa kura 14,030 baada ya kupata kura 15,379 dhidi ya kura 1,349 za Kijo.

Katika Jimbo la Nyanza, Paul Bomani aliyekuwa akitumia alama ya jembe alipata kura 28,738 na kumshinda kwa kura 18,317 mpinzani wake, Daniel Madaha Machemba, aliyepata kura10,421.

Katika Jimbo la Hombolo, Job Malecela Lusinde (alama ya nyumba) alipambana na Paulo Mukombola (alama ya jembe). Lusinde alipata kura 28,839 na Mukombola alipata kura 8,262. Lusinde aliibuka mshindi kwa kumpita mpinzani wake kwa kura 20,577.

Jimbo la Muheza Erasto Andrew Mang’enya (alama ya jembe) aliyepata kura 28,168 alishinda kwa kura 19,986 dhidi ya Juma Ali Bakari (alama ya nyumba) aliyepata kura 8,182.

Jimbo la Mwibara aliyeshinda ni Stephen Wasira Masatu aliyepata kura 10,446 dhidi ya kura 9,213 za mpinzani wake, Thomas Mwiyenjwa. Huko Lushoto Josephat Kifunta Mandia (kura 18,576) alimshinda Ibrahim Joseph Shemdoe aliyepata kura 10,498.

Katika Jimbo la Hai, Israel Eninawinga (alama ya jembe) aliyepata kura 31,091 alimshinda Solomoni Simbo (alama ya nyumba) aliyepata kura 3,980. Katika Jimbo la Rombo, aliyekuwa mbunge wake, Alphonse Maskini (alama ya jembe), ambaye alipata kura 11,719, alishindwa na Leonce Ngalai (alama ya nyumba) aliyepata kura 17,691. Kura zilizoharibika zilikuwa ni 1,276. Kwa Jimbo la Vunjo mshindi alikuwa ni Bi Kaanasia Mtenga (alama ya jembe) ambaye alipata kura 19,461 dhidi ya kura za mpinzani wake, Mosha Antony Mafole (alama ya nyumba) aliyepata kura 16,262.

Katika uchaguzi huo Mwalimu Nyerere alitangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Chifu Adam Sapi Mkwawa, kuwa ameshinda uchaguzi huo kwa asilimia 95 ya kura zote zilizopigwa. Idadi ya kura zilizomkataa, kwa mujibu wa Mwenyekiti Mkwawa, ni 108,828. Kura zilizoharibika ni 74,388.

Novemba 5, 1970, Mwalimu Nyerere aliapishwa kwa mara nyingine kuwa Rais wa Tanzania. Siku ya kuapishwa Rais aliwasamehe jumla ya wafungwa 3,484.

Kesho katika safu hii tutaona jinsi baraza la mawaziri la 1970 lilivyoundwa.