Wahamiaji haramu tisa wa Kenya wakamatwa Dodoma Tanzania

Kandama wa polisi mkoa wa Dodoma Gilles Muroto akiwaonyesha baadhi ya wahamiaji haramu walikamatwa mkoani Dodoma Wakitokea nchini Kenya. Picha na Nazael Mkiramweni

Muktasari:

  • Polisi nchini Tanzania linawashikilia raia tisa wa Kenya wakituhumiwa kuingia nchini humo kinyume cha sheria. Uchunguzi dhidi yao unaendelea na watafikishwa mahakamani pindi taratibu zitakapokamilika.

Dodoma. Polisi mkoani Dodoma nchini Tanzania limewakamata wahamiaji haramu tisa ambao ni raia wa Kenya kwa kosa la kuingia nchini kinyume cha sheria katika matukio mawili tofauti.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Februari 15, 2000, Kamanda wa polisi mkoani Dodoma, Gilles Muroto amesema wahamiaji hao kati yao watatu ni raia wa Kenya wenye asili ya Somalia waliokamatwa katika Kijiji cha Mtera wilaya ya Mpwapwa, Dodoma.

Amewataja raia hao ni Abdirahman Mohamed (25) Luul Mohamed (30) na Hawa Gedow (18) wakitokea nchini Kenya kwenda nchini Zambia kupitia Mkoa wa Songwe Tanzania .

Muroto amesema raia hao walikuwa kwenye gari lenye namba za usajili T. 248 AWA aina ya Nissan Patrol rangi nyekundu likiendeshwa na Kelvin Mpoli mkazi wa Himo mkoani Kilimanjaro ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari Kifaru Wilaya ya Mwanga mkoani himo akiwa na Cathbert Kirita (58) mmiliki wa gari hilo.

Katika tukio lingine, wahamiaji haramu sita walikamatwa Februari 3, 2020 kata ya Haneti Wilaya ya Chamwino wakitokea mkoani Arusha kwenda Mbeya.

Amesema walikuwa wakitumia usafiri wa gari la abiria lenye namba T.858 DAP kampuni ya Capricon inayofanya safari zake kutoka Arusha kwenda Mbeya.

Amewataja majina yao kuwa ni; Abdifatah Mohames (12), Ikran Mohames (17), Abdullah Mohamed (11), Farhiya Fahar (33), Abdlaziz  Mohamed (13) na Mohamed Mohamed (23) wote raia wa nchi ya Kenya ambao walikuwa na hati za kusafiria za Kenya, “zilitiliwa mashaka na kubainika kuwa waliiingia nchini kinyume cha sheria.”

Amesema wahamiaji hao watafikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika.