Wahitimu Mzumbe watakiwa kutotembelea na bahasha kutafuta ajira

Friday December 6 2019

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe nchini Tanzania, Profesa  Lughano Kusiluka amesema hatarajii kuona wahitimu wa chuo wakizunguka na bahasha yenye nakala ya vyeti wakitafuta kazi wakati wamejengewa uwezo  na ujuzi wa kujiajili.

Profesa Kusiluka ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Desemba 6, 2019 wakati wa mahafali ya sita ya Chuo hicho kampasi ya Dar es Salaam yaliyohudhuriwa na Mkuu wa Chuo cha Mzumbe Jaji mkuu  mstaafu Barnabas Samatta.

Makamu huyo amewasihi wahitimu hao kutumia vyema fani zao ili kuijenga Tanzania ya viwanda ambayo ni azma ya Serikali ya awamu ya tano ili kulipeleka Taifa kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

"Kwa fani ambazo mmezisomea hapa chuoni, ni dhahiri kwamba mmepata elimu, ujuzi na maarifa ya kutosha ya kushiriki kwenye ajenda hii muhimu ya kitaifa. Hututaki wahitimu wa Mzumbe wazunguke na bahasa yenye nakala za vyeti kutafuta ajira," amesema Profesa Kusiluka.

Katika mahafali hayo wahitimu 445 walitunukiwa shahada za umahiri wa fani mbalimbali kati ya hao wanawake 236 sawa na asilimia 53.0 na wanaume 209 sawa na asilimia 47.

Kaimu mwenyekiti wa baraza chuo hicho, Pius Maneno amewataka wahitimu hao kutumia elimu na ujuzi walioupata chuoni hapo kutatua changamoto zinazoikabili jamii sambamba na kuwa wabunifu.

Advertisement

"Kuhitimu kwenu leo mnakuwa sehemu ya nguvu kazi ya Taifa letu, jamii ya Watanzania inawategemea kwa elimu, ujuzi weledi na maarifa mliyoyapata hapa chuoni. Mtaleta mabadiliko chanya katika maisha yenu, familia na jamii zitakazowazunguka," amesema Maneno.

Advertisement