Waitara ampa rungu DC Sabaya fedha mfuko wa jimbo la Mbowe

Muktasari:

  • Naibu waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara ametembelea jimbo la Hai linaloongozwa na Freeman Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania na kutoa maagizo kadhaa ikiwamo matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo.

Hai. Naibu waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara amemwagiza Mkuu wa Wilaya (DC) ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya kutumia Sh42 milioni za mfuko wa jimbo hilo ambazo zimekaa kwa miaka miwili bila kutumika.

Waitara amesema fedha hizo zilitolewa mwaka wa fedha 2018/19 ambazo hadi sasa hazijapangiwa matumizi yoyote kinyume na taratibu za matumizi ya fedha hizo.

Maagizo hayo aliyatoa jana Jumatano Januari 8, 2020 wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri  ya wilaya ya Hai pamoja na wananchi wa kijiji cha Longoi alipokwenda kutembelea ujenzi wa kituo cha afya.

Alisema fedha hizo ni kwaajili ya kuchochea miradi ya maendeleo. Jimbo la Hai linaongozwa na Freeman Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Katika mazungumzo yake, Waitara alisema, "mwenye mamlaka ya kupangia fedha za mfuko ni DC na mkurugenzi na sio mbunge kama anavyofanya mbuge wa Jimbo hili Freeman Mbowe."

Alisema fedha hizo zilitakiwa zitumike tangu mwaka 2019 hadi sasa hazijatumika hivyo ni kosa na kwamba kwa kutumia mamlaka aliyonayo amemtaka Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kutawanya fedha hizo kwenye miradi ya maendeleo vijijini.

"DC mwagize mkurugenzi atawanye fedha hizo, wananchi watume maombi na DC uzisimamie zitumike kwenye matumizi yanayotakiwa," alisema  Waitara.

Aidha alisema Mbowe hana mamlaka ya kupanga matumizi ya fedha hizo bali  anatakiwa kuchukua matatizo ya wananchi na kuyawasilisha bungeni .

Alisema Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema amekuwa mtoro wa kufanya kazi za wananchi na badala yake amekuwa akifanya matumizi ya fedha hizo kwa njia ya simu jambo  ambalo sio sahihi.

"Sabaya ndie Mkuu wa Wilaya ya Hai na ndiyo mwenye mamlaka ya kuamua nini kifanyike ndani ya wilaya hii," alisema Waitara aliyewahi kuwa Chadema kabla ya kujiuzulu na kutimia CCM.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Hai, Ole Sabaya alisema endapo mtu yoyote  atafanya matumizi mabaya ya fedha za wananchi atamfyatua na kumtupilia mbali baada ya kupewa nguvu hiyo na naibu waziri huyo.

"Mheshimiwa naibu waziri kituo hiki cha afya ulicho kitembelea leo ni jitihada za kuhakikisha wananchi wa ukanda huu wa tambarare wanakumbukwa katika shughuli za maendeleo na tayari mpaka sasa kiasi cha Sh338 milioni zimechangwa kutoka vyama vya ushirika na wananchi na fedha hizo zipo katika akaunti iliyo funguliwa," alisema Sabaya.

Aidha Sabaya alimtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuhakikisha ndani ya wiki moja wananchi wanatuma maombi ya matumizi ya fedha hizo na zigawanywe  kwa kufuata sheria za matumizi ya fedha hizo.