Waitara awaonya wanaohamasisha vurugu uchaguzi Serikali za mitaa

Friday November 8 2019

Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara akijibu

Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara akijibu swali bungeni wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma leo 

By Sharon Sauwa,Mwananchi [email protected]

Dodoma. Naibu Waziri wa Tamisemi nchini Tanzania, Mwita Waitara amewaonya wanaohamasisha vurugu kwa sababu ya kutoridhishwa na mchakato wa uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Waitara ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Novemba 8, 2019 bungeni mjini Dodoma baada ya mbunge wa Singida Kaskazini (CCM),  Justine Monko kutaka kauli ya Serikali baada ya Chadema kujitoa kushiriki uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 24, 2019.

“Uamuzi wa Chadema unawakosesha haki za msingi wananchi kwa mujibu wa katiba na mfumo wa vyama vingi, je Serikali ina kauli gani na kadhia hii inayoendelea nchini,” amehoji Monko.

Akijibu swali hilo, Waitara amesema uchaguzi wa Serikali za mitaa utafanyika kama kawaida.

Amewataka wananchi  waliojiandikisha na vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huo kuendelea na taratibu nyingine.

Waitara amesema kesho ni siku ya mwisho ya kuwasilisha malalamiko ya wagombea walioenguliwa, kwamba waliojiondoa hawana haja ya kulalamika.

Advertisement

“Tulieleza mara kadhaa watu wenye sifa ya kutoa pingamizi ni wagombea,  wenzetu walilalamika katika mitandao na mitaani na Serikali iamue! Serikali inafanya kazi kwa barua na mawasiliano hakuna document (nyaraka) mezani hatuwezi kujadili jambo,” amesema.

Amesema kuna matangazo yanatolewa katika mitandao kuwa wananchi wasishiriki katika shughuli za maendeleo, akibainisha kuwa mwenye mamlaka ya kutoa maagizo nchini ni Rais John Magufuli na si kiongozi yoyote wa chama.

Pia Waitara amewaagiza wakuu wa wilaya nchini kuwachukulia hatua za kisheria wanaohisi hawakutendewa haki na kufanya fujo.

Naye mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amehoji sababu za uchaguzi wa Serikali za mitaa kutofanyika pamoja na uchaguzi mkuu, Mwita kujibu kuwa suala hilo ni la kisheria wamelipokea na watalifanyia kazi.

Advertisement