Wakatoliki waandamana DRC kupinga ufisadi

Monday October 21 2019

 

Kinshasa. Wafuasi wa Kanisa Katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wameandamana kupinga ufisadi na ukosefu wa haki za kisheria nchini humo.

Maandamano hayo yaliitishwa na Kamati ya Walei ya kanisa hilo ambao wamewataka wananchi wa DRC kuingia mitaani kwa ajili ya kupinga mambo hayo.

Walei hao wanaaminika kuwa ndiyo waliomshinikiza aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila kuachana na azma yake ya kugombea muhula wa tatu madarakani.

Hiyo ni mara ya kwanza kwa Kamati ya Walei kuitisha maandamano chini ya utawala mpya wa Rais wa sasa, Felix Tshisekedi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, Walei hao wameitisha maandamano hayo ya amani baada ya kupotea kwa Dola za Marekani 15 milioni kutoka benki ya Taifa ya DRC na kuwekwa katika benki ya biashara kabla ya kutoweka kabisa.

Licha ya kilio cha wananchi ambao waliwataka wahusika wachukuliwe hatua. Hata hivyo, Rais Tshisekedi pamoja na Mahakama ya nchi hiyo hawajatoa maelezo ya kutosha kwa umma kuhusu suala hilo.

Advertisement

Akizungumza na BBC, mmoja wa viongozi wa Wakatoliki hao, Isidore Ndaywele Nziem alisema wanakerwa na ufisadi uliokithiri, ukiukaji wa sheria kwa kutowaadhibu wahalifu na kudorora wa mfumo mzima wa sheria nchini humo .

Kamati hiyo imevipongeza vyama vya kisiasa, makundi ya raia na mashirika yasiyo ya kiserikali waliopaza sauti zao kuunga mkono maandamano hayo.

Katika taarifa yake, kamati imewataka waandamanaji kutojihusisha na aina yoyote ya ghasia, kuchoma moto mataili na kuweka vizuizi vya barabarani, kutotumia lugha matusi, kutorusha mawe na vitu vingine au kufanya uporaji wowote wa mali wakati wa maandamano hayo.

Advertisement