Wakazi Dar watakiwa kujitokea viwanja vya Zakhem Mbagala kusajili laini za simu

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amewataka wakazi wa Mkoa huo kujitokeza katika viwanja vya Zakhem vilivyopo eneo la Mbagala kwa ajili ya kusajili laini zao za simu.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amewataka wakazi wa Mkoa huo kujitokeza katika viwanja vya Zakhem vilivyopo eneo la Mbagala kwa ajili ya kusajili laini zao za simu.

Kesho Jumatatu Januari 20, 2020 ndio siku ya mwisho ya usajili wa laini za simu kwa alama za vidole.

Makonda amesema katika viwanja hivyo kampuni zote za simu zitakuwa zikitoa huduma za usajili kwa wananchi hadi saa 11 jioni.

Makonda ametoa kauli hiyo leo Jumapili Januari 19, 2020 kupitia video fupi iliyorekodiwa na kusambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

“Takwimu nilizonazo watu milioni 7 wenye namba na vitambulisho vya Nida hawajasajili laini zao. Habari njema kwa wakazi wa Dar es Salaam, tumewaandalia eneo hili kwa ajili ya kuwapa fursa ya kusajili laini zao.”

“Kampuni zote za simu zitakuwepo. Simu ni yako na laini ya kwako na Tanzania ni Taifa lako,  kwa nini usitumie fursa hii kukamilisha mchakato huu utakaolinda usalama wa mali zako na Taifa,” amesema Makonda.