Wakili Msando alipa Sh5 milioni kwa niaba ya Rais Magufuli, bado Sh364,814

Wakili Alberto Msando akikabidhi risiti za malipo ya bili kwa Rais wa Chama cha  madaktari Tanzania, Dk Elisha Osati

Muktasari:

  • Wakali Alberto Msando amekabidhi Sh5 milioni kwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dar es Salaam kama malipo ya bili ya marehemu Sabina Loita ambayo Rais wa nchi hiyo, John Magufuli aliahidi kuilipa

Dar es Salaam. Wakili wa kujitegemea nchini Tanzania, Alberto Msando ameipatia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Sh5 milioni kama malipo ya matibabu ya marehemu Sabina Loita ambaye mtoto wake alimlilia Rais wa nchi hiyo, John Magufuli hospitalini hapo siku chache zilizopita.

Tukio hilo lilitokea Agosti 11, 2019 wakati Rais Magufuli akitoka kuwatembelea majeruhi 43 wa ajali ya lori la mafuta ya petroli lililoanguka na kulipuka eneo la Msamvu mkoani Morogoro Agosti 10,2019.

Baada ya binti huyo kuomba msaada kwa Rais Magufuli, kiongozi huyo wa nchi  aliiagiza hospitali hiyo kumruhusu kuchukua mwili wa ndugu yake huku akiomba fedha hiyo adaiwe yeye.

Leo Ijumaa Agosti 23,2019, Msando wakati wa kukabidhi risiti za malipo yaliyofanywa, amesema tukio hilo lilimsukuma kuomba Watanzania kuchangia bili hiyo badala ya kumuacha Rais Magufuli ailipe yeye mwenyewe.

“Alisema adaiwe yeye na wala hakutaka kutumia madaraka yake kama Rais kwa sababu pia alikuwa na uwezo wa kusema apewe mwili wa mama yake bila kudaiwa ila alitaka kuilipa yeye, kutokana na hilo nilimpigia simu na kumuambia kuwa nitailipa,” amesema Msando

“Nilitumia mtandao wangu wa kijamii wa Instagram kuomba mchango kutoka kwa Watanzania, zoezi ambalo lilifanyika kwa siku tatu na watu walijitoa kulingana na kile walichonacho,” amesema wakili huyo

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji MNH, Profesa Lawrence Museru amesema baada ya Rais kuahidi kulipa bili hiyo waliitayarisha na kumpelekea Ikulu.

“Bili ilikuwa ya Sh5,364, 814 lakini leo kupitia ndugu yetu Sh5 milioni imelipwa hivyo leo tutapeleka barua nyingine kumuambia kuwa kiasi kingine tayari kimelipwa na imebakia Sh364,814 na atakapolipa tu zoezi hili litafungwa rasmi,” amesema Profesa Museru.