Wakili aieleza mahakama anachougua Mbowe

Muktasari:

Kesi inayowakabili viongozi tisa wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania imeshindwa kuendelea kwa hatua ya ushahidi baada ya mshitakiwa wa kwanza kuwa mgonjwa.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam nchini Tanzania imeshindwa kuendelea na kesi inayowakabili viongozi wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Kesi hiyo ambayo ilikuwa iendelee leo Jumanne Novemba 26, 2019 kwa utetezi imeshindwa baada ya wakili wa utetezi kueleza afya ya Mbowe bado sio nzuri.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala amedai mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa afya Mbowe bado sio nzuri kwa kuwa bado anaumwa.

"Mbowe bado anaumwa, ameruhusiwa kutoka hospitali Ijumaa Novemba 22, 2019 na anasumbuliwa na Dengue, high blood pressure (shinikizo la juu la damu) pamoja na malaria," amedai Kibatala

Amedai  kesi hiyo ni ya jinai mshtakiwa asingekuja kwa kuwa  bado ni mgonjwa toka ameruhusiwa ametakiwa kupumzika.

Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi amedai walipokea taarifa ya mshtakiwa wa kwanza ikiambatanishwa na taarifa ya daktari.

Alidai kama mshtakiwa aliruhusiwa tangu Ijumaa Novemba 22,2019 na kwa utaalamu wa madaktari ina maana mgonjwa huyo atakuwa amepona.

"Hatuoni sababu ya kuahirisha kesi hii Mahakama ilipanga kusikiliza, kuiahirisha inabidi kuwa na uthibitisho utakaoonyesha sababu ya kuahirisha kama atakuwa ametoka hospitali toka Ijumaa atakuwa kapumzika vya kutosha," amedai Nchimbi

Hakimu Simba alieleza kuwa afya ya mtu ni muhimu kuliko vitu vingine na hivyo kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 28 na 29, 2019.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni  Katibu Mkuu, Dk Vicent Mashinji, Naibu katibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Wengine ni wabunge wa chama hicho, John Heche (Tarime Vijijini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Esther Matiko (Tarime Mjini), Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya wa Bunda Mjini.

Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 12 ikiwemo la uchochezi, kufanya mkusanyiko usio halali na kukaidi amri ya jeshi la polisi.