Wakili akwamisha kesi ya Mpemba wa Magufuli

Muktasari:

Kesi ya kukutwa na meno ya tembo inayomkabili, Yusuf Ali Yusuf maarufu kama ‘Mpemba wa Magufuli na wenzake imekwama kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Alhamisi Novemba 14, 2019.

Dar es Salaam. Kesi ya kukutwa na meno ya tembo inayomkabili, Yusuf Ali Yusuf maarufu kama ‘Mpemba wa Magufuli na wenzake imekwama kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Alhamisi Novemba 14, 2019.

Kesi hiyo ilipangwa kuendelea  na ushahidi leo upande wa mashtaka lakini kutokana na wakili anayeendesha shauri hilo kupata udhuru ilishindikana.

Yusuf na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka manne ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo ya Sh785.6milioni.

Wakili wa Serikali, Slyvia Mitanto mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema, “upande wa mashtaka tunaye shahidi  lakini kwa bahati mbaya wakili anayeendesha kesi hii amepata udhuru na kushindwa  kufika mahakamani. Tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.”

Hakimu Simba baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka amesema kesi hiyo ni ya muda mrefu na kuutaka upande wa mashtaka kuleta mashahidi kesi hiyo itakapotajwa tena.

Kuhusu washtakiwa watatu waliomuandikia barua mkurugenzi wa mashtaka (DPP) kuomba msamaha, upande wa mashtaka  umedai utafutilia suala kujua suala hilo limefikia wapi.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 28, 2019 na washtakiwa kurudishwa rumande.

Mbali na Yusuph, washtakiwa wengine katika kesi hiyo  ni Charles Mrutu, maarufu Mangi Mapikipiki na mkazi wa Mlimba, Morogoro; Benedict Kungwa, mkazi wa Mbagala Chamazi;  Jumanne Chima, maarufu JK na mkazi wa Mbezi;  Ahmed Nyagongo, dereva na mkazi wa Vikindu-Mkuranga na Pius Kulagwa ambaye ni  mfanyabiashara na mkazi wa Temeke.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kujihusisha na mtandao wa ujangili, katika kesi ya uhujumu uchumi namba 53/2016.

Miongoni mwa shtaka moja kati ya manne yanayowakabili washtakiwa hao ni kujihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya dola 180,000 sawa na Sh 392,817,600 bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.