Wakili awapinga mkurugenzi, kamishna Nec mahakamani

Friday November 22 2019

 

By James Magai, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakili wa kujitegemea Alex Masaba amefungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu akipinga uteuzi wa Mkurugenzi mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec)Dk Wilson Charles Mahera na kamishna wa tume hiyo, Omar Mapuri.

Katika kesi hiyo namba 30 ya mwaka 2019, wakili Masaba ambaye anajiwakilisha mwenyewe anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa uteuzi wa viongozi hao wa Nec ni batili kwa kukiuka na kuvunja masharti ya Katiba ya nchi na sheria ya Nec.

Pia anaomba mahakama itamke kuwa wateule hao wameshindwa kuzingatia wajibu wao wa masharti ya Katiba kwa kukubali uteuzi huo kwani kwa mujibu wa Ibara ya 26(1) (2) kila raia anawajibu wa kuzingatia kulinda na kuhifadhi Katiba na sheria za Tanzania.

Akifafanua uteuzi huo kikatiba, Wakili Masaba anafafanua kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 74(15)(a-d), wajumbe wa Nec watateuliwa miongoni mwa watu wenye uzoefu wa kutosha na utendaji wa shughuli za tume hiyo.

Lakini anadai kwa nyakati tofauti Rais wa Tanzania amewateua viongozi hao katika nafasi hizo wakati bado ni wanachama hai wa chama cha siasa, yaani Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wakili Masaba anadai kuwa mkurugenzi huyo wa Nec, Septemba 2012 aliteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Halmashsuri Kuu ya Taifa ya CCM kutoka wilayani Butiama, mkoani Mara.

Advertisement

Pia anabainisha kuwa Mapuri alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuanzia 2005 hadi 2007 na 2008 mpaka 2010 na kwamba wakati fulani miaka ya 1985 mpaka 2000 aliwahi kuwa mtumishi wa Serikali katika nafasi ya uwaziri, Bara na Zanzibar.

Wakili Masaba anadai kuwa Nec ni taasisi ya kisheria ambayo haiko chini ya mamlaka wala ushawishi wa mhimili wowote kati ya mihimili mitatu yaani, Serikali, Bunge na Mahakama au chama chochote cha siasa.

Anasisitiza kuwa pia ni idara huru ambako watu wote wanaohusika na uendeshaji wa uchaguzi wanapigwa marufuku kujiunga na chama chochote cha siasa.

Pia anabainisha kuwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi, mahakama inazuiliwa kuchunguza jambo lolote lililofanywa na Nec katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa masharti ya kikatiba, isipokuwa tu pale inapoendesha shughuli zake kinyume cha Katiba.

Hivyo anadai kuwa wateule hao kutokana na nafasi zao hizo za kisiasa ndani ya CCM, ni watu wasio na uzoefu katika kusimamia na kuendesha uchaguzi.

Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watu linaloongozwa na Jaji Dk Benhajj Masoud, ilitajwa mahakamani hapo jana kwa mara ya kwanza na mahakama ikaipa Serikali siku saba kuwasilisha mahakamani kiapo kinzani kujibu hoja za wakili huyo.

Mahakamani hapo jana Mwanasheria Mkuu wa Seikali ambaye ni mdaiwa wa kwanza, aliwakilishwa na Yohana Marko na mwenzake wakati NEC (mdaiwa wa pili), Mahera (mdaiwa wa tatu ) na Mapuri (mdaiwa wa nne) waliwakilishwa na Wakili Elizabeth Kimako.

Advertisement