Wakulima Tanzania waundiwa mkakati wa kuwanufaisha

Muktasari:

Katika kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wakulima, Benki ya NMB imejiwekea lengo la kufungua akaunti zaidi ya  300,000 kwa mwaka 2020.

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wakulima, Benki ya NMB imejiwekea lengo la kufungua akaunti zaidi ya  300,000 kwa mwaka 2020.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ruth Zaipuna amesema mpango huo unalenga kuhakikisha wakulima wanapata malipo yao kupitia mfumo rasmi wa fedha  na kuchangia katika kukuza huduma jumuishi za fedha nchini Tanzania.

Zaipuna ameeleza hayo mkoani Mwanza katika hafla ya kutambulisha kitabu cha Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kiitwacho Maisha Yangu, Kusudi Langu.

Ameeleza kuwa NMB inatambua umuhimu wa sekta ya kilimo katika uchumi wa nchi na ndiyo sababu imeamua kuwageukia wakulima

Amesema miaka 22 tangu kuanzishwa kwa benki hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa wafanyabiashara na sasa wanataka fursa hiyo iwafikie pia wakulima.

Mkapa amepongeza mafanikio ya benki hiyo na kusifu uamuzi wa serikali yake wa kuibinafsisha.

“Nafarijika kuona NMB ni miongoni mwa benki kubwa yenye mtandao mkubwa nchini ikihudumia wananchi wa kawaida hadi vijijini,” amesema Mkapa