Walichokisema Mbowe, Maalim Seif kushambuliwa Tundu Lissu

Muktasari:

Viongozi wa vyama vya upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe na Maalim Seif Sharif Hamad wamezungumzia tukio la kushambuliwa kwa kiongozi mwenzao Tundu Lissu na kumshukuru Mungu kwa kumponya kutokana na kadhia hiyo aliyoipata Septemba 7, 2017.


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe na Mshauri Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad wamemshukuru Mungu kwa maendeleo ya afya ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Lissu alishambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma nchini Tanzania akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge leo Jumamosi ya Septemba 7, 2019 amefikisha miaka miwili akiwa ughaibuni.

Baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kisha usiku wa siku hiyo hiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya hadi Januari 6, 2018 alipopelekwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi ambako bado yuko huko mpaka sasa.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ametumia akaunti yake ya Twitter kuzungumzia siku tukio hilo na kilichoendelea.

“Mungu ni yuleyule, jana, leo na hata milele, habadiliki, tulimuomba, akatenda, tunamuomba, anatenda na tutamuomba, ataendelea kutenda, kama alivyotenda miaka miwili iliyopita siku kama ya leo 7 Septemba.”

“Wanadamu huwa tunaiwaza kesho hatujui itakuwaje, lakini Mungu alishatujua hata kabla ya kuzaliwa kwetu na alijua mwisho wetu,” amesema Mbowe

Mbunge huyo wa Hai amesema, “Na kwa sababu tunamuamini Mungu na tunamuomba na kwa kuwa ni mwaminifu na hachelewi wala hawahi hapo ndipo unapojua Mungu ndiye Injinia wa maisha ya kila mmoja wetu.”

Amesema, “Mungu tunakushukuru kwa kumponya Lissu, kumtunza, kumlinda kutoka kwenye mikono ya yule mwovu shetani, kila mwanadamu anayeishi basi ndani yake kuna kusudi lake Mungu, kama hakuna kusudi lake Mungu, Septemba 7, 2017, Lissu angepoteza maisha, lakini Mungu ndiye mlinzi wa maisha ya kila mtu.”

“Hakuna anayeweza kutoa uhai wa mtu kama Mungu hajapanga. (God is the same always and never changes). Mungu ibariki Dunia, Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania. (Hebrews 13:8),” ameongeza

Ujumbe kama huo umetolewa na Maalim Seif aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar aambaye ameandika katika Twitter yake kuwa, “Leo tunakumbuka miaka miwili tokea kufanyika jaribio la kumuua #TunduLissu aliyepigwa risasi 36, 16 zikiwa zimempata mwilini.”

“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumnusuru na kifo na kuendelea kumponesha. Kauli yetu ni moja tu kwake na kwa Watanzania wote: Hakuna kusalimu amri,” ameongeza Maalim Seif aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF)