Walimu ‘makada wa CCM’ wampiga chenga Dk Bashiru

Muktasari:

Wakati katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akiwapiga marufuku kuanzisha umoja kwa kutumia jina la chama hicho tawala, walimu wamebadili jina la kongamano waliloandaa na kushikilia msimamo wa kuanzisha umoja huo wa wakereketwa.

Dar/Dodoma. Wakati katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akiwapiga marufuku kuanzisha umoja kwa kutumia jina la chama hicho tawala, walimu wamebadili jina la kongamano waliloandaa na kushikilia msimamo wa kuanzisha umoja huo wa wakereketwa.

Dk Bashiru alitoa kauli hiyo baada ya kuitishwa kwa Kongamano la Umoja wa Walimu Makada wa CCM lenye lengo la kumpongeza Rais John Magufuli kwa kile walichoelea kuwa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama hicho, lakini jana waliiambia Mwananchi kuwa watabadilisha jina la kongamano hilo na kulifanya kuwa kama la kawaida.

Alitoa onyo hilo juzi zikiwa zimebaki takribani siku kumi kabla ya kongamano hilo kufanyika Septemba 7 jijini Dodoma, huku wakitangaza angekuwa mgeni rasmi anatarajia kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama.

Akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya katika majimbo ya Dar es Salaam juzi, Dk Bashiru alisema “mimi sina kundi linaloitwa shirikisho au jukwaa la walimu. Kuna matawi ya CCM. Mwalimu anayetaka siasa aende kwenye tawi au kwenye jumuiya, ukitaka ya wanawake, vijana na wazazi unakaribishwa”.

“Sitaki kusikia utambulisho huu, walimu kama wanataka kufanya kazi za kitaaluma waende kwenye vyama vya wafanyakazi, wakija kwenye chama makundi ni hayo. Huji kama mwalimu, unakuja kama mwanaCCM,” alisema mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alisema kuna maadili ya ualimu yanayogongana na uanachama kwa sababu ukiwa darasani unafundisha watoto wa Taifa hili, bila kujali itikadi za wazazi wao, na kwamba ukiwa mwalimu unafundisha taifa zima.

“(Mwalimu) Ni mtumishi wa umma unalipwa na walipakodi ambao ni Watanzania wa vyama vyote. Sasa nasikia kuna upepo mbaya unapita huko, makatibu wa mikoa na wilaya msitambue makundi hayo kwa utambulisho huo. Tambueni makundi ya wanachama wakulima na wafanyakazi,” alisema.

Msimamo huo wa Dk Bashiru umepokewa kwa maoni tofauti ya walimu hao.

Mratibu mkuu wa kongamano hilo, Mwalimu Yasini Mponda alisema “kongamano lipo palepale” ila kinachofanyika watabadilisha jina kutoka Umoja wa Waalimu Makada wa Chama cha Mapinduzi na sasa watajiita “Walimu Nchini Tanzania”.

Mponda, ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Kigongwe iliyoko mjini Dodoma, alisema uamuzi wa kubalisha jina hilo unatokana na kuwepo kwa walimu wengi ambao si makada wa chama hicho kuwa na nia ya kushiriki kongamano hilo pamoja na utekelezaji wa kauli ya Dk Bashiru.