Walimu Zanzibar walipwa Sh2.2 bilioni

Wednesday December 4 2019

By Haji Mtumwa, Mwananchi [email protected]

Unguja. Leo Jumatano Desemba 4, 2019 Baraza la Wawakilishi limeelezwa kuwa Sh2.2 bilioni zimetumika kulipa posho na likizo kwa walimu 22,623 kuanzia mwaka 2011 hadi 2019.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Desemba 4, 2019 na naibu Waziri wa  Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohamed Said katika kikao cha baraza hilo wakati akijibu swali la mwakilishi wa Paje (CCM),  Jaku Hashim Ayoub.

Katika swali lake Ayoub alitaka kujua changamoto zinazowakabili walimu zilizotatuliwa.

Akijibu swali hilo naibu waziri huyo amesema hakuna mwalimu anayedai posho na likizo.

Amesema wizara hiyo imelipa malimbikizo ya mshahara ya Sh315.3 milioni kuanzia kwama 2011 hadi 2015.

Amesema walimu  2,974 wameajiriwa mwaka 2011 hadi 2019, kwamba 3,109 wameruhusiwa kwenda kwenye masomo ya muda mfupi na mrefu.

Advertisement

“Nichukue fursa hii kuwapongeza walimu kwa uvumilivu ninawaomba  waendelee na wizara inatatua changamoto zao hatua kwa hatua. Tunakishukuru chama cha walimu Zanzibar (Zatu) kwa kushirikiana na Wizara yetu kuhakikisha tunafikia malengo ya Serikali,” amesema.

Advertisement