Walimu madarasa ya awali wapewa mbinu

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Haki Elimu, Dk John Kalage akimkabidhi cheti, Mwalimu Ajira Hongoli  cheti baada ya kumaliza mafunzo ya Elimu ya awali yanayoitwa mwanzo mzuri

Muktasari:

Wakati wanafunzi wa madarasa ya awali wakijiandaa kuanza masomo mwakani 2020, zaidi ya walimu 40 wamenolewa na kupewa mbinu bora za kufundisha watoto ikiwamo kuwafanya rafiki.

Dar es Salaam.  Walimu wa madarasa ya awali wametakiwa kuwafanya watoto rafiki zao ili iwe rahisi kuelewa kile wanacho wafundisha darasani.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Prestige jijini Dar es Salaam, Ajira Hongoli amesema hayo baada ya kumaliza mafunzo ya elimu ya awali yanayoitwa ‘mwanzo mzuri’ ambayo yametolewa kwa ushirikiano baina ta Taasisi ya Haki Elimu, Chuo Kikuu cha Mkwawa na Chuo Kikuu cha Via cha nchini Dermark.

“Tuwafanye watoto rafiki zetu, tujifunze kutoka kwao nimeweza kufanya hilo ninaloongea baada ya kupata haya mafunzo, sina mtoto anayeniogopa kwenye darasa langu, wote wamekuwa rafiki zangu,” amesema Hongoli.

Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Elimu, Dk John Kalage amesema mafunzo hayo yamelenga kuwaongezea walimu hao ujuzi baada ya tafiti mbalimbali kuonyesha watoto wasipopata elimu ya awali hawawi na mwanzo mzuri wa kujifunza.

Dk Kalage amesema wanatarajia kuwafikia walimu kutoka shule 127 za Serikali na binafsi ili matokeo ya watoto kujifunza yasaidie kuendelea kuandaa mbinu bora za kujifunza.

“Mafunzo haya ni kama utafiti tunataka kuona matokeo ya shule ambazo walimu wamefundishwa mbinu bora za kuwafundisha watoto kutoka kwenye mradi huu wa mwanzo mzuri,” amesema Dk Kalage.

Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mkwawa mkoani Iringa, Dk Jacline Amani amesema walimu hao wamekuwa wakipata mafunzo kwenye chuo hicho kila baada ya miezi mitatu ili kuwanoa.

“Tunachotaka ni kuona ubora wa elimu kwenye nchi yetu ya Tanzania, tunaamini walimu wakishirikiana katika kubadilishana uzoefu na kupewa mafunzo, ubora wa elimu utaongezeka,” anasema.

Naye Mratibu wa Chuo Kikuu cha Via nchini Tanzania, Dk Suma Kaare amesema zipo mbinu za kumfanya mtoto apende shule na aelewe masomo darasani, na hizo ndizo walizokuwa wanafundisha.

“Elimu ya awali inamtengeneza mtoto kuwa sehemu ya dunia, inampa mwanzo mzuri wa masomo yake na walimu wanaofundisha lazima wawe wamenolewa kuweza kutoa elimu hiyo kwa watoto,” amesema Dk Kaare.