Breaking News

Walimu watano kizimbani kwa kuvujisha mitihani

Friday October 16 2020

 

By Twalad Salum

Misungwi. Walimu watano wa shule ya msingi Seeke, wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wamefikishwa mahakamani wakituhumiwa kuvujisha mitihani ya Taifa ya darasa la saba.

Waliofikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Misungwi juzi ni Amos Alphonse (35), Ramadhani Athumani (30), John Magina (39), Islam Rahibu (26) na Christina Majura (52).

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi, mwendesha mashitaka wa Polisi, Ramsoney Salehe alidai washtakiwa hao walikula njama na kuvujisha mitihani ya Taifa wa kuhitimu darasa la saba.

Salehe alidai kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Oktoba 7, wakiwa eneo la shule ya msingi Seeke.

Mitihani inayodaiwa kuvujishwa na washtakiwa ni ya masomo ya Hisabati na Kiswahili.

Walikana mtuhuma hizo. Washtakiwa Alphonce na Majura waliachiwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya dhamana ya Sh5 milioni na mali isiyohamishika.

Advertisement

Washtakiwa wengine walipelekwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Kesi itatajwa Oktoba 20.

Wanafunzi wa darasa la saba nchini walifanya mitihani ya kuhitimu elimu hiyo Oktoba 7 na 8.

Advertisement