Walioambukizwa corona Tanzania wafikia 25

Muktasari:

Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amesema walioambukizwa ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona nchini wamefikia 25 baada ya mgonjwa mwingine mmoja kuongezeka leo Jumatano Aprili 8, 2020.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amesema walioambukizwa ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona nchini wamefikia 25 baada ya mgonjwa mwingine mmoja kuongezeka leo Jumatano Aprili 8, 2020.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo inamnukuu Ummy akisema kuwa mtu huyo mwenye umri wa miaka 51 ni mkazi wa Dar es Salaam na yuko katika kituo maalum cha uangalizi wa tiba jijini humo.

“Hadi sasa watu 25 wamethibitika kuwa na maambukizi ya corona tangu kuanza kwa ugonjwa huu nchini. Wagonjwa hawa ni pamoja na wale waliotolewa taarifa kutoka Zanzibar ambapo kati ya hao waliopona ni watano na mmoja amefariki.”

“Tangu turipoti mgonjwa wa kwanza wa corona nchini hadi kufikia leo saa 5 asubuhi jumla ya watu 789 waliokutana na wagonjwa wanafuatiliwa kwa karibu. Kuanzia Machi 24, 2020 hadi sasa wasafiri 2,181 wamewekwa karantini na kati yao wasafiri 324 wamemaliza siku 14 za uangalizi,” amesema Ummy