Waliofariki ajali ya lori la mafuta Morogoro yafikia 75

Muktasari:

Idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali ya moto iliyotokea Jumamosi Agosti 10, 2019 mkoani Morogoro imefika 75 baada ya wengine wanne kufariki dunia katika  Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali ya moto iliyotokea juzi Jumamosi Agosti 10, 2019 mkoani Morogoro nchini Tanzania imefika 75.

Idadi hiyo imeongezeka baada ya wengine wanne kufariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam walikohamishiwa kwa matibabu zaidi.

Hospitali hiyo ilipokea majeruhi 46 kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya matibabu zaidi hata hivyo, saba kati yao wamefariki.

Akizungumza leo Jumatatu Agosti 12, 2019 Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano MNH Aminiel Aligaesha amesema kwa sasa idadi ya majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu ni 39.

“Tumepoteza wenzetu wengine wanne na miili yao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hivyo kama kuna ndugu wa karibu waje kwa ajili ya kuwatambua ndugu zao,” amesema Aligaesha.

Kuhusu hali za majeruhi mkuu huyo wa kitengo cha mawasiliano amesema wanaendelea vizuri na wapo wanaoonyesha matumaini.

“Watanzania tuendelee kuwaombea wenzetu na niwaambie tu kuwa wanaendelea vizuri na wataalamu wetu wanaendelea kuhakikisha kuwa majeruhi wanapata huduma stahiki ili afya zao ziweze kuimarika,” amesema

“Tunaomba pia ndugu jamaa na marafiki wajitokeze kwa ajili ya kutambua miili ya ndugu zao, lakini pia tunakaribisha wale ambao ndugu zao wamelazwa waje kuwaona,” ameongeza