Waliofariki ajali ya moto Morogoro wafikia 95

Sunday August 18 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Idadi ya waliokufa kutokana na ajali ya moto iliyotokea mkoani Morogoro imefikia 95 baada ya majeruhi mmoja aliyekuwa amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kufariki jana usiku Jumamosi  Agosti 18, 2019.

Hadi jana mchana waliofariki katika ajali hiyo walikuwa 94 baada ya majeruhi mwingine kati ya 21 waliokuwa wamelazwa MNH kufariki.

Jana alasiri hospitali hiyo ilipokea majeruhi mwingine kutoka hospitali ya Mkoa wa Morogoro na kufanya idadi yao kuwa 21 lakini sasa wamebaki 20 baada ya mwingine kufariki jana saa nne usiku.

Ajali hiyo ilitokea Agosti 10, 2019 katika mtaa wa Itingi, Msamvu barabara ya Morogoro-Dar es Salaam baada ya lori la mafuta kupinduka na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta.

Akizungumza leo Jumapili Agosti 18, 2019 mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa MNH, Aminiel Aligaesha amesema aliyefariki dunia ni Rajabu Ally.

Amebainisha kuwa wagonjwa 20 wapo katika chumba cha uangalizi maalum (ICU), madaktari wanafanya jitihada kuokoa maisha yao.

Advertisement

Amewaomba watu wa kada mbalimbali kuendelea kuchangia damu kuwasaidia majeruhi hao.

Advertisement